Kiambaa kuamua mwelekeo wa Nyoro kisiasa – Wadadisi

Kiambaa kuamua mwelekeo wa Nyoro kisiasa – Wadadisi

Na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA mustakabali wa kisiasa wa Gavana wa Kiambu James Nyoro utaamuliwa na matokeo ya chaguzi ndogo za eneo bunge la Kiambaa na wadi ya Muguga zinazofanyika kesho.

Baada ya chama cha Jubilee kubwagwa katika uchaguzi mdogo wa Juja, uliofanyika Mei mwaka huu, wadadisi wanasema chaguzi hizi mbili ni kufa kupona kwa Gavana Nyoro kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Ingawa chaguzi hizi ndogo, haswa ule wa Kiambaa unasawiriwa kama mapambano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, mwenye wasiwasi zaidi ni Gavana Nyoro,” anasema mchanganuzi wa kisiasa, Bw Charles Munyoi.

Kulingana naye ushindi wa mgombeaji wa Jubilee Kariri Njama katika eneo la Kiambaa utamweka Bw Nyoro katika nafasi bora ya kuhifadhi kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa upande mwingine, anaongeza, kushindwa kwa Jubilee kutazima ndoto ya gavana huyo kuhifadhi kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao, kwani ataonekana kama kiongozi asiye na ushawishi mashinani.

Hii ndio maana juzi gavana huyo alikuwa mwepesi kupuuzilia mbali kura ya maoni iliyoonyesha kuwa mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (ADC), John Njuguna Wanjiku ataibuka mshindi katika eneo bunge la Kiambaa.

Alisema utafiti huo ulidhaminiwa na kuendeshwa na vigogo wa UDA kama sehemu ya mikakati wa kupata sababu ya kupinga matokeo baada ya mgombea wa Jubilee Kariri Njama kutangazwa mshindi.

“Tuna hakika kwamba tutashinda Kiambaa. Nawaomba mpuuzilie kura hiyo ya maoni inayoonyesha kuwa wanaongoza,” akasema.

“Nia yao ni kwamba baada sisi kushinda, watasema tumeiba,” Gavana Nyoro akasema alipowahutubia waombolezaji katika hafla ya mazishi eneobunge la Gatundu Kaskazini.

Tayari gavana huyo ameanza kuingiwa na wasiwasi kwamba huenda akapoteza kiti chake cha ugavana endapo chama cha Jubilee kitapoteza kiti hicho ambacho kilisalia wazi baada ya kifo cha Paul Koinange mnamo Machi mwaka huu.

Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi na Mbunge wa Thika Mjini Patrick Wainaina, “Wajango” ni miongoni mwa wanasiasa ambao tayari wametangaza azma ya kuwania kiti cha ugavana wa Kiambu.

You can share this post!

Sifuna asema Rais Kenyatta hahitaji kuunganisha vinara wa...

Aliyeuawa kinyama alituzwa na Rais 2016