Habari Mseto

Kiambu tayari kwa upanzi wa miti ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Mazingira

June 4th, 2019 2 min read

 Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya na shirika la PELUM wanajiandaa kupanda takriban miti 1,000 eneo la Lari, Uplands Juni, 5 2019, kuadhimisha siku ya mazingira ulimwenguni.

Chuo hicho cha Mount Kenya kimejitolea kushirikiana na PELUM kupanda miti kwa wingi huku wananchi wakihimizwa kufuata mkondo huo.

Wakati uo huo pia MKU itashirikiana na shirika la Msalaba Mwekundu kupanda miti 2,000 katika sehemu ya Happy Vally Pavalion mjini Thika.

Meneja wa soko na mauzo wa Mount Kenya Bw Boniface Murigi alisema chuo hicho limejitolea kulinda mazingira huku wakihimiza wakazi wa Landless wapande miti kwa wingi.

Kulingana na ripoti kutoka kwa wasimamizi wa chuo hicho inasema wameamua kuzingatia mwelekeo huo kwa minajili ya kufanikisha shughuli hiyo.

Mkurugenzi wa Shirika la PELUM Bw Zachary Makaya, amesema wanatarajia kupanda miti eneo la Lari, huku lengo lao likiwa ni kuona ya kwamba hali ya mazingira inaimarika katika Kaunti ya Kiambu.

“Tutashirikiana na wakazi wa eneo hili ili kufanikisha shughuli yenyewe. Hata tumetuma ujumbe kwa machifu wazungumze na wakazi hao ili siku ya mazingira ionekane kuwa ya manufaa,” alisema Bw Makaya.

Kulingana na mipango iliyoko, shughuli hiyo itafanyika sehemu za Lari katika maeneo ya Aberdare ambapo wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi wakati huo.

Mipango iliyowekwa inaonyesha ya kwamba wakati wa shughuli hiyo miti 1,000 itapandwa awamu ya kwanza, halafu baadaye pia wananchi wataongezwa mingine 1,000 itakayopandwa siku hiyo.

Serikali ya kaunti

Wakati wa siku ya mazingira, waziri wa mazingira na maafisa wakuu wa Kaunti ya Kiambu, watahudhuria ili kujumuika na wengine katika upanzi wa miti.

Kulingana na shirika a PELUM shughuli hiyo inawiana na mpango wa serikali kuona ya kwamba miti inapandwa kwa asilimia 10 kote nchini.

PELUM Kenya ina ushirikiano wa karibu na mashirika mengine 50 na wakulima wadogowadogo wapatao 2 milioni ambao wamebadilisha maisha yao kwa maswala ya kilimo na utafiti.

Shirika la PELUM lina mipango maalum kuona ya kwamba wanawapa wakulima mawaidha jinsi ya kuendesha kilimo kwa njia ya kisasa.

Wakati huo pia PELUM inawafunza wakulima hao jinsi ya kuongeza ujuzi katika kilimo chao cha kila siku.

Wanahimizwa kuelewa umuhimu wa utunzaji mazingira katika shughuli zao za kilimo.