Habari MsetoSiasa

Kiambu yateua Naibu Gavana mpya

February 19th, 2020 1 min read

SIMON CIURI na WANDERI KAMAU

GAVANA wa Kiambu Dkt James Nyoro, Jumatano alimteua Dkt Joyce Wanjiku Ngugi kuwa naibu gavana mpya.

Dkt Ngugi ni mkwewe aliyekuwa mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Joseph Ngugi.

Dkt Nyoro pia alifanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri. Dkt Nyoro aliapishwa kama gavana mpya wa kaunti hiyo mwezi uliopita.

Alikuwa akihudumu kama Kaimu Gavana baada ya mtangulizi wake, Bw Ferdinard Waititu kuzuiwa kufika afisini na mahakama kutokana na kesi ya ufisadi inayomkabili.

Baadaye, Bw Waititu alipoteza wadhifa wake mwezi uliopita, baada ya Seneti kupiga kura kuidhinisha hatua ya Bunge la Kaunti hiyo kumwondoa uongozini.

Muda mfupi baada yake kuchukua uongozi, viongozi walianza kumshinikiza kumteua mwanamke kama naibu gavana.

Spika wa Bunge la Kaunti Bw Stephen Ndichu alisema alikuwa amezungumza na gavana kuhusu pendekezo hilo, ambapo alilikubali.

Dkt Nyoro amejiunga na magavana kadhaa nchini ambao wamewateua wanawake kama manaibu gavana.

Baadhi yao ni Mutahi Kahiga (Nyeri) na Kivutha Kibwana (Makueni) ambao wamewateua Dkt Carol Karugu na Bi Adelina Mwau mtawalia.

Bw Ngugi alifariki mnamo 2014 baada ya kuanguka nyumbani kwake katika mtaa wa Runda jijini Nairobi.

Dkt Ngugi alikuwa ametangaza nia ya kuwania wadhifa huo baada ya kifo cha mumewe, lakini akajiondoa baada ya mbunge wa sasa, Moses Kuria kukosa mpinzani yeyote.

Hatua hiyo sasa inazima uwezekano wowote kwa Bw Waititu kutetea nafasi yake, ikizingatiwa alikuwa amewasilisha kesi mahakamani kupinga hatua ya kuapishwa kwa Dkt Nyoro kama gavana.

Tangu kuchaguliwa kwake mnamo 2017, Bw Waititu amekuwa akiandamwa na msururu wa kesi za ufisadi.

Kwenye kesi inayomkabili, anadaiwa kufuja zaidi ya Sh588 milioni kupitia utoaji kandarasi.