Na SAMMY KIMATU
KIANGAZI ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa zaidi ya miaka 60 katika maeneo ya Milima ya Iveti kaunti ya Machakos kinaathiri wakazi na mifugo mwezi huu.
Naibu Mkuu wa chifu eneo la Mutituni, Bw Musyoki Mutua Mallei aliambia Taifa Leo kwamba walioathirika zaidi ni wakulima na mifugo.
“Kawaida, mlima iveti unajulikana na kwa kuwa na chemichemi nyingi zinazowezesha wenyeji kukuza upanzi wa mboga na matunda. Tangu mwaka 2022 kufikia mwezi huu, chemichemi nyingi zimekauka kabisa,” Bw Musyoki akasema.
Aliongeza kwamba kufuatia maji kupungua katika visima, wakazi hulazimika kupanga foleni usiku kuanzia saa tano angalau mtu apate mtungi mmoja wa lita 20 wa maji ya kunywa.
Maeneo mengine tajika kwa ukulima wa unyunyizaji yanayokumbwa na ukame ni pamoja na Ngelani, Kisekini, Lita, Kaviani, Misakwani, Mumbuni, Mua, Kiima Kimwe, Mbukoni na Mung’ala.
Bw Mutuku Maweu, Mkulima katika eneo la Kiteini alisema wafungaji wanalazimika kununua nyasi inayouzwa Sokoni Mutituni kwa Sh300 kwa kila kifungu.
Kufuatia hali hiyo, serikali imerai wenyeji kukumbatia upanzi wa miti ili kukabili changamoto zilizoko kufuatia Tabianchi.
Bw Musyoki aliwatahadharisha wenyeji kuhusu mikasa ya moto inayoweza kutokea wakati huu wa kiangazi.
“Watu wawe makini kuwakisha moto kiholela. Wanaotupa vipande vya sigara kiholerla wameonywa sawia na wanaowakisha majiko na wale wote huwasha moto kuchoma matofali ni lazima muwe chonjo kabisa msisababishe ajali za moto,” Bw Musyoki akaongeza.
Vilevile, wenyeji wanaiomba serikali ya kaunti kuchimba visima zaidi ili kukabiliana na hali iliyopo ndiposa kuokoa maisha ya watu na mifugo.
Maeneo ya Machakos yanatambuliwa kwa kilimo cha kahawa, parachichi, plamu, nyanya na sukumawiki ambazo hukuzwa kwa wingi.