Kianjokoma: Polisi mahabusu waomba DPP azimwe

Kianjokoma: Polisi mahabusu waomba DPP azimwe

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA sita wa polisi wanaozuiliwa kufuatia vifo vya ndugu wawili katika Kaunti ya Embu wanaomba Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) azuiwe kuwafungulia mashtaka ya mauaji.

Polisi hao pia wanaomba mahakama kuu iamuru miili ya wavulana hao ifukuliwe kisha ifanyiwe upasuaji “wakiwakilishwa na mawakili na daktari wao.”

Sita hao wanasema ripoti ya Dkt Johansen Oduor ilionyesha ndugu hao walikufa kutokana na kichapo kwa kifaa butu.

“Washukiwa hao hawakuwakilishwa na wakili au daktari wao katika shughuli ya upasuaji wa miili yao ili kukubaliana na uamuzi uliofikiwa,” akasema wakili Danstan Omari.

Sita hao wanadai vijana hao waliruka kutoka kwenye gari la polisi walipokuwa wanapelekwa katika kituo cha polisi cha Manyatta wakiwa na mahabusu wengine wanane.

Washukiwa hao wanaomba mahakama iamuru uchunguzi ufanywe kubaini kilichosababisha vifo vya wavulana hao.

“Polisi wanaozuiliwa hawakuwaua wavulana hao kamwe bali waliruka kutoka katika gari la polisi likienda kasi kisha wakakata roho,” akasema wakili Bw Omari.

Bw Omari aliambia Taifa Leo ushahidi uliorekodiwa na mahabusu walioshikwa pamoja na wahanga hao wawili ni kwamba “waliwaona wakijirusha kutoka kwenye gari la polisi huku wakidhani wameponyoka na kukwepa kufikishwa kortini.”

Polisi wanaozuiliwa ni Koplo Benson Mbuthia, Koplo Consolata Kariuki, Nicholas Sang Cheruiyot, Martin Msamali Wanyama, Lilian Cherono Chemuna na James Mwaniki.

Pia mahakama inaombwa iamuru washukiwa hao warudishiwe simu zao wawasiliane na benki zao watoe pesa za kuwalipia karo watoto wao.

Washukiwa hao wanasema hawana pesa za kukimu mahitaji ya familia zao na pia ada ya mawakili kwa vile hawawezi kutoa pesa kwa akaunti kwa vile “simu zilichukuliwa na polisi.”

Washukiwa hao wanachunguzwa kwa lengo la kuwashtaki kwa mauaji ya Benson Njiru Ndwiga, 22, na Emmanuel Mutura Ndwiga, 19.

Bw Omari amesema kinyume cha vile ilidaiwa kuwa polisi waliteketeza gari lililokuwa limewabeba vijana hao, ni wananchi waliokuwa na hasira walioliteketeza wakati wa kukabiliana na waandamanaji.

Wakili huyo alisema kuwa baada ya wavulana hao kujirusha, polisi wa idara ya trafiki ndio walichunguza kesi hiyo na hata kulipeleka kukaguliwa kisha likarudishwa katika kituo cha polisi kufanya kazi nyingine.

“Ushahidi uliopo ni kuwa vijana hao hawakuuawa msituni na maiti zao kupepelekwa mochari. Walijiua kwa kujirusha kutoka kwa gari la polisi,” alisema Bw Omari.

Polisi hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Agosti 30 watakapofikishwa kortini kujibu mashtaka ya mauaji.

You can share this post!

Serikali yajipanga kuchanja mamilioni

Wanafunzi wazimia shuleni kwa njaa