Kiarie apendekeza M-Pesa na Safaricom ziende njia panda

Kiarie apendekeza M-Pesa na Safaricom ziende njia panda

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Dagoretti Kusini John Kiarie sasa anataka huduma za kutuma na kupokea pesa kupitia simu za M-Pesa na Airtel Money zitenganishwe na kampuni husika za mawasiliano.

Akiongea wakati wa kongamano la kutoa uhamasisho kwa wabunge katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi, Bw Kiarie alisema kuwa huduma hizi zinafaa kusimamiwa na Benki Kuu Nchini (CBK).

“Huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia za simu kama vile M-Pesa na Airtel Money zinafaa kusimamiwa na CBK. Kwa upande mwingine huduma za simu nazo zisimamiwe na Mamlaka ya Mawasiliano (CA),” akapendekeza Bw Kiarie ambaye ni mbunge wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Ikiwa pendekezo la Bw Kiarie litatekelezwa, kampuni ya Safaricom itagawanywa kuwili ili kutengenisha huduma za M-Pesa na huduma za mawasiliano.

Kampuni ya Airtel pia itagawanywa kwa njia iyo hiyo ili kutengenesha hudumu za Airtel Money na kitengo cha mawasiliano kwa njia ya simu ya mkononi.

Bw Kiarie alisema ni makosa kwa kampuni za mawasiliano kuendesha shughuli za benki nje ya sheria za benki.

“Shughuli zote za kutuma fedha, kukopa fedha kwa kutozwa riba zinafaa kusimamiwa na CBK lakini sio jinsi hali ilivyo sasa chini ya huduma za M-Pesa na Airtel Money,” akaeleza.

Akiongea kuhusu pendekezo hilo, Gavana wa CBK Patrick Njoroge alisema suala hilo lina mantiki na akapendekeza Bunge la Kitaifa lipitishe mswada wa kufanikisha hatua hiyo.

“Ninyi wabunge ndio watunga sheria. Kwa hivyo, ni wajibu wenu kutunga sheria ya kuwezesha utekelezaji wa pendekezo hili lenye busara,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mbappe afokewa vikali na wafuasi wa PSG

Tenisi ya Ferdinand Omanyala yavutia chipukizi 120

T L