Kibai, Rono watwaa dhahabu Olimpiki ya Viziwi

Kibai, Rono watwaa dhahabu Olimpiki ya Viziwi

Na VICTOR OTIENO akiwa Caxias do Sul, Brazil

SYMON Kibai alitimiza lengo lake la kuzoa mataji mawili kwenye Olimpiki ya Viziwi nchini Brazil, Jumamosi.

Kenya ilishinda medali nane katika riadha (dhahabu mbili, fedha nne na shaba mbili) Jumamosi pekee.

Mafanikio hayo yalishuhudia Kenya ikifikisha jumla ya medali 24 (dhahabu tano, fedha nane na shaba 11) kabla ya mbio za marathon zilizoratibiwa jana alasiri.

Katika makala ya 2017 mjini Samsun nchini Uturuki, Kenya, ambao ni miamba wa riadha barani Afrika, walikamata nafasi ya tisa kwa jumla ya medali 16 (dhahabu tano, fedha tano na shaba sita).

Kibai, ambaye alikuwa ametetea taji la mbio za mita 10,000 hapo awali, alihifadhi ubingwa wa mbio za mita 5000 baada ya vita vikali dhidi ya Mkenya mwenzake Ian Wambui.

Wambui, ambaye mapema juma lililopita alinyakua dhahabu ya mita 1500 na kuapa kupokonya Kibai taji la mita 5,000, alikuwa bega kwa bega na Mkenya huyo mwenzake ugani Sesi Centro, wakibadilishana uongozi mara kadhaa mvua ikinyesha.

Lakini Kibai alionyesha Wambui kivumbi katika mzunguko wa mwisho alipoongeza kasi na kutwaa taji kwa dakika 14:14.81.

Wambui aliambulia nishani ya fedha (14:24.27) naye Mswidi Otto Kingstedt akafunga tatu-bora (14.44.19).

Elikana Rono alinyakua dhahabu ya mita 800 kwa 1:54.75 alifuatiwa na Mhispania Jaime Martinez (1:54.88) na Michal Kulpa kutoka Poland (1:54.91).

Grancy Kandagor aliridhika na medali ya shaba ya mita 5, 000 kwa finals Grancy Kandagor kwa dakika 18:16.44 nyuma ya Sara-Elise Ruokonen (17:33.03) na Lourdes Juarez (17:33.91).

Wakenya Beryl Wamira, Linet Nanjala Sharon Bitok na Pamela Atieno walinyakua fedha ya mita 400 kupokezana vijiti nao Isaac Atima, George Waweru Charles Muthama na Simon Menza wakaridhika na shaba ya kitengo hicho upande wa wanaume.

Beryl Wamira akionyesha nishani ya shaba aliyotunukiwa baada ya kukamilisha mbio za mita 200. PICHA | HISANI

Ilikuwa medali ya nne ya Wamira. Ana fedha mbili na shaba mbili.

Sharon Jeptarus na Rebecca Matiko walivuna medali ya fedha na shaba katika mita 800 mtawalia. Anastasia Sydorenko alibeba taji.

You can share this post!

Shule ya Sheikh Khalifa kufanya hafla maalum ya kuomboleza...

Yaibuka naibu rais alikuwa amefanya uamuzi wa mbunge wa...

T L