Habari MsetoMakalaSiasa

Kibaki alivyofichwa ndani ya stoo chafu serikali ikipinduliwa

July 31st, 2019 3 min read

Na VALENTINE OBARA

KENYA Alhamisi inahitimisha miaka 37 tangu jaribio la mapinduzi ya serikali iliyoongozwa na Rais Mstaafu Daniel arap Moi, katika mwaka wa 1982.

Katika jaribio hilo la mapinduzi lililoanza alfajiri ya Agosti 1, 1982 na kudumu kwa karibu saa 12 likisimamiwa na wanajeshi wa ngazi za chini wa kikosi cha wanahewa, raia wasiopungua 200 walisemekana kufariki sawa na wanajeshi karibu 100.

Tofauti na jinsi mengi yamesemwa kuhusu jinsi maafisa wa usalama walimtorosha Mzee Moi kutoka nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru hadi mahali salama mwituni, hali ya makamu wake wa rais, Bw Mwai Kibaki wakati huo haijapewa uzito.

Wakati wanajeshi waasi wakiongozwa na Hezekiah Ochuka walipofanya uvamizi kwa mashirika mbalimbali ya kiserikali kwa lengo la kupindua utawala, Rais Mstaafu Kibaki alikuwa nyumbani kwake Othaya, Nyeri. Ochuka alinyongwa baadaye alipopatiana na hatia ya uhaini.

Ingawa fununu zilisema kulikuwa na njama ya kumng’oa Bw Moi ili Kibaki akabidhiwe mamlaka ya kuongoza taifa, baadhi ya maafisa walihofia huenda yeye pia angelengwa na waasi hao.

Kwa msingi huu, ilibidi aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Kati uliokuwepo wakati huo, Bw David Musila, achukue hatua za dharura kumwepushia madhara Bw Kibaki.

Kwenye kitabu chake cha ‘Seasons of Hope’ ambacho kilizinduliwa mapema mwaka huu, seneta huyo wa zamani wa Kaunti ya Kitui, alisema Bw Kibaki alikuwa nyumbani kwake Othaya baada ya kufungua maonyesho ya kilimo Nyeri pamoja na Moi.

Moi alienda bomani kwake Kabarak baada ya hafla hiyo.

“Nilimpigia simu kuuliza kama alikuwa salama nikawaambia ninamtuma afisa wa polisi wa ngazi za juu kumchukua. Ilikuwa ni muhimu kwamba nitume mtu atakayemwamini,” akaeleza Bw Musila.

Aliamua kumtuma Bw Samuel Wathome ambaye alikuwa afisa wa kitengo maalumu cha polisi katika mkoa huo, na Bw Kibaki alimfahamu vyema.

Kulingana naye, Bw Kibaki alikuwa na wasiwasi walipozungumza kwa simu na alitaka kujua jambo lililokuwa likiendelea lakini hata Bw Musila hakujua mengi isipokuwa yaliyokuwa yametangazwa kwenye kituo cha redio cha taifa, VoK ambacho kilitekwa na wanajeshi waasi.

Bw Wathome aliunda kikosi kidogo cha maafisa wa polisi walioandamana naye hadi kwa Bw Kibaki wakiwa wamejihami kwa silaha kali, wakafanikiwa kumfikisha mjini Nyeri salama baada ya kumwamrisha kufuata kila agizo atakalopewa kwa usalama wake.

“Alipofika Nyeri, niligundua alikuwa na wasiwasi kwa sababu ya matukio yaliyoibuka. Sikushangaa kwa sababu alikuwa ni makamu wa rais wa serikali iliyokuwa inapinduliwa na kama kulikuwa na watu ambao waasi wangependa kukamata, bila shaka angekuwa miongoni mwa wa kwanza kwenye orodha yao,” Bw Musila asema kwenye kitabu chake.

Baada ya kumfikisha Nyeri, changamoto sasa ilikuwa ni kutafuta mahali pa kumficha kwa muda. Iliamuliwa apelekwe Nyeri Club.

“Tulipata chumba kidogo kilichokuwa ni stoo chafu, nikamfungia humo ndani. Nilijua waasi hawangefikiria kumtafuta makamu wa rais mahali kama hapo,” akasema.

Lakini alibadili mawazo yake baada ya muda mchache kwani alitambua haikuwa sawa kumfungia mtu mwenye hadhi kama ya Bw Kibaki ndani ya stoo chafu.

Hapo ndipo iliamuliwa Bw Kibaki apelekwe nyumbani kwake karibu na Hospitali ya Mlima Kenya mjini Nyeri, na nyumba hiyo ilindwe saa zote, usiku na mchana. Jukumu la kumpikia Bw Kibaki lilikuwa mikononi mwa mke wa Bw Musila.

Baada ya jaribio la mapinduzi kuzimwa mwendo wa saa kumi na mbili jioni na jeshi la kikosi cha wanahewa walioegemea kwa serikali wakiongozwa na Meja Jenerali Mahamoud Mohammed, Bw Musila alimleta Bw Kibaki nyumbani kwake kwa chajio na kumpigia simu Mzee Moi kumwarifu kuhusu jinsi hali ilivyokuwa upande wake.

Anasema Bw Kibaki alikuwa akisikiliza kwa makini mazungumzo hayo, na kabla kukata simu, makamu wa rais akaomba azungumze na rais lakini Moi akakataa kwa sauti ya ukali.

“Kibaki alikuwa amesimama kando yangu akisubiri nimkabidhi simu, lakini kwa mshangao wangu, rais alinijibu kwa ukali kwamba hakutaka kuzungumza na makamu wa rais.”

Ilibidi amdanganye Bw Kibaki kwamba Mzee Moi hakutaka kuongea zaidi kwa vile alikuwa amechoka. Bw Kibaki hakuteta.

Asubuhi iliyofuata ndipo Bw Kibaki alisindikizwa na kikosi kikubwa cha usalama hadi Nairobi kuhudhuria mkutano wa baraza la mawaziri.

Inaaminika tukio hilo ndilo lilimbadilisha sana Bw Moi akaanza kuwa mtawala wa kiimla.

Rais huyo mstaafu alikuwa amekamilisha miaka minne pekee mamlakani, baada ya kuchukua usukani 1978 kufuatia kifo cha rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta mnamo Agosti 22 mwaka huo.

Utawala wa Moi uliodumu kwa miaka 24 ulishtumiwa kwa visa vingi vya ukiukaji wa haki za kidemokrasia ikiwemo mauaji ya viongozi wa kisiasa kwa njia zisizoeleweka, wanasiasa wa upinzani kukamatwa na kufungwa gerezani bila hatia ambako waliteswa, na ufujaji wa mali ya umma.

Hata hivyo, Kenya imefanikiwa kupiga hatua katika masuala ya uongozi hasa kupitia kupitishwa kwa katiba mpya mwaka wa 2010, baada ya Chama cha Kanu kilichoongozwa na Bw Moi kushindwa kwenye uchaguzi wa urais katika mwaka wa 2002.

Katika uchaguzi huo, Bw Kibaki ndiye alishinda urais kupitia Chama chake cha PNU kilichokuwa chini ya muungano wa NARC na kumbwaga Rais Uhuru Kenyatta ambaye alipeperusha bendera ya Kanu.

Muungano huo mkubwa wa kisiasa ulijumuisha pia Chama cha Liberal Democratic Party (LDP) ambacho kiliongozwa na Bw Raila Odinga, ambaye sasa anaongoza Chama cha ODM.

Bw Odinga alikuwa miongoni mwa viongozi wa kisasa ambao walidaiwa kuhusika katika kupanga njama ya mapinduzi hayo, ingawa dai hili halijawahi kuthibitishwa kisheria.