MakalaSiasa

MWAI KIBAKI: Mwanasiasa msomi aliyevumilia na kukwea ngazi hadi Ikulu

April 3rd, 2019 4 min read

Na KENYA YEARBOOK

IWAPO majina ya viongozi walioiletea nchi hii sifa yataorodheshwa kwenye kumbukizi ya taifa, basi jina la Rais Mstaafu Mwai Kibaki haliwezi kukosekana katika orodha hiyo.

Bw Kibaki alichaguliwa Rais wa tatu wa Kenya katika uchaguzi Mkuu wa mwezi Disemba mwaka wa 2002 kupitia uungwaji mkono wa viongozi waliokuwa wamekiasi chama tawala cha KANU na wengine wa upinzani.

Kiongozi huyu mwenye sifa za kupigiwa mfano kwa muda wa miaka 50 aliyoshiriki siasa, alizaliwa Novemba, 15 1931 katika eneobunge la Othaya, Kaunti ya Nyeri.

Alikuwa mwanawe Kibaki Githinji na Teresia Wanjiku huku mamisheneri waliombatiza akiwa kijana wakimpa majina Emilio Stanley ingawa aliacha kutumia majina hayo baadaye.

Akiwa mdogo, Bw Kibaki alijiunga na shule za kimisheni za Gatuya-ini na Karima kisha akaendeleza masomo hayo katika Shule ya Mathari ambayo kwa sasa inafahamika kama Nyeri High kutoka darasa la nne hadi sita kati ya mwaka wa 1944 hadi 1946.

Kama wanafunzi wengine kutoka jamii za kiafrika enzi hizo, Bw Kibaki alisomea useremala kwa kuwa sheria za shule zilihitaji kila mwanafunzi kuwa na ujuzi huo ili kuunda samani na kukarabati majengo ya shule.

Kutokana na uchochole wa familia yake, Bw Kibaki alifanya kazi ya utingo mjini Othaya ili kupata fedha za kujikimu shuleni.

Darasani, Bw Kibaki alikuwa mwerevu sana na hilo lilidhihirika alipofuzu vizuri katika mtihani wa shule ya msingi na kuhitimu kujiunga na shule ya upili ya Mangu mwaka 1947. Aliendeleza ufanisi huo kwa kuibuka wa kwanza shuleni humo kwenye mtihani wa wa kitaifa wa mwaka wa 1950.

Ingawa aliazimia kuwa mwanajeshi baada ya masomo hayo kutokana na kushajishwa na ukakamavu wa wapiganiaji walioshiriki vita vya pili vya dunia, hatua ya serikali ya kikoloni kuzipiga marufuku jamii za Agikuyu, Embu na Meru kujiunga na idara hiyo ilizima ndoto za Bw Kibaki ya kujiunga na kikosi hicho kinachotoa ulinzi kwa taifa.

Akiwa na kiu ya kuendeleza masomo yake, Bw Kibaki alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kusomea shahada katika Uchumi, Historia na Sayansi ya Kisiasa. Mwaka wa 1955 alifuzu kwa kupata alama za juu zaidi ndipo akapata kazi kama naibu meneja wa mauzo kwenye tawi la kampuni ya mafuta ya Shell nchini Uganda.

Kung’aa kwake katika anga za elimu kulimpelekea kupata ufadhili wa masomo katika Chuo cha hadhi cha kutoa Mafunzo ya Kiuchumi cha London alikosomea shahada ya uzamili kwenye masuala ya fedha.

Mnamo mwaka wa 1958, alifuzu vizuri na akarejea Uganda kama mhadhiri wa kozi ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Makerere alikofundisha hadi mwaka wa 1960 kisha akarejea nchini kujiunga na chama cha KANU.

Aliingia katika asasi ya ndoa kwa kumwoa Lucy Muthoni ambaye alikuwa mwanawe mzee wa kanisa Katoliki mwaka wa 1962. Wawili hao wamejaliwa watoto wanne; Judy Wanjiku, Jimmy Kibaki, David Kagai na Tony Githinji.

Safari ya kisiasa ya Bw Kibaki ilianza 1963 alipochaguliwa kama mbunge wa Doonholm jijini Nairobi kupitia chama cha KANU. Eneobunge hilo lilibadilishwa jina na kuitwa Bahati miaka ya 60 na tena likapewa jina jipya la Makadara ambalo bado linatumika hadi leo.

Nyota ya kisiasa ya Bw Kibaki ilianza kung’aa baada ya Uhuru pale Rais wa kwanza Jomo Kenyatta, alipomteua kama Naibu Waziri katika Wizara ya Fedha na pia Mwenyekiti wa Tume ya Mipango ya Kiuchumi mwaka wa 1963.

Kutokana na utaalamu wake, Mzee Kenyatta alimpandisha cheo hadi akawa Waziri wa Biashara 1966 kisha baadaye 1969 akamhamisha hadi Wizara muhimu ya Fedha.

Ni katika kipindi hiki alipojivunia sifa kedekede kwa kusimamia vizuri uchumi wa nchi na ukuaji wa hali ya juu ikashuhudiwa. Rais wa Benki ya Dunia Robert MacNamara aliwahi kunukuliwa akimtaja kama moja wa wasomi wenye ujuzi mkubwa Barani Afrika wanaoweza kubadilisha uchumi wa bara hili.

Alichaguliwa kwa mara nyingine kama Mbunge wa Bahati kwenye uchaguzi wa mwaka wa 1969 na akahudumu hadi 1974 alipoitikia wito wa wakazi wa Othaya wa kumtaka awanie uchaguzi wa mwaka huo katika eneobunge lake la nyumbani.

Baada ya kuhamisha siasa zake kutoka jiji la Nairobi hadi Nyeri, Bw Kibaki alichaguliwa kwa urahisi kama mbunge wa Othaya kwenye chaguzi zilizofuatia za 1979, 1983, 1988, 1992, 1997, 2002 na hatimaye 2007 alipostaafu siasa.

Nyota ya jaha iliendelea kumulika Bw Kibaki alipoteuliwa Makamu wa Rais mwaka wa 1978 na Rais Daniel Torotich Arap Moi baada ya kifo cha Mzee Kenyatta mwaka huo. Ingawa hivyo, aliendelea kushikilia wadhifa wake wa Waziri wa Fedha chini ya utawala wa Moi hadi 1988 alipopigwa kalamu kama Makamu wa Rais na kuhamishwa kuhudumu kama Waziri wa Afya.

Baada ya katiba kubadilishwa kuondoa utawala wa chama kimoja, Bw Kibaki aliushangaza ulimwengu kwa kujiuzulu kutoka serikalini mwaka wa 1991 na kukiunda chama cha Democratic Party(DP) alichotumia kuwania urais.

Hata hivyo juhudi zake za kutwaa kiti cha Urais mwaka wa 1992 na 1997 ziligonga mwamba baada ya Rais Moi kukishinda kiti hicho kutokana na mgawanyiko mkubwa kati ya viongozi wa upinzani kama Jaramogi Oginga Odinga, Kenneth Matiba, Raila Odinga, Martin Shikuku miongoni mwa wengine.

Ndoto ya Bw Kibaki ilitimia Disemba mwaka wa 2002 aliposhinda urais kwa asilimia 62 za kura baada ya kuungwa mkono na viongozi wa upinzani pamoja na waasi wa chama cha KANU.

Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, George Saitoti, Moody Awori, William Ole Ntimama waliohama KANU baada ya Rais Moi kuidhinisha Uhuru Kenyatta kama mgombeaji wa Urais waliunda chama cha Liberal Democratic Party(LDP) na kuungana chama cha National Alliance Party of Kenya(NAK) kilichokuwa kikongozwa na Bw Kibaki, Michael Wamalwa Kijana na Charity Ngilu na kushinda uchaguzi huo wa Disemba 27, 2002.

Hatimaye Bw Kibaki aliapishwa kama Rais wa tatu wa Kenya Disemba 30, 2002 akiwa kwenye kiti cha magurudumu kutokana na ajali mbaya aliyokumbana nayo katika barabara ya Machakos-Nairobi akitoka kampeni maeneo ya Kitui.

Alichaguliwa kukamilisha hatamu yake ya uongozi mwaka wa 2007 kwenye uchaguzi tata uliopingwa vikali na mpinzani wake Raila Odinga aliyedai aliibiwa ushindi.

Katika muda wa miaka 50 alizoshirikia siasa za nchi, Bw Kibaki ametajwa na wengi kama kiongozi mnyamavu ambaye msimamo wake kuhusu masuala kadhaa ya kitaifa haujitokezi waziwazi kwa urahisi.

Mwaka wa 1974, jarida la Times lilimworodhesha miongoni mwa watu 100 duniani wenye uwezo wa kuongoza mataifa yao.