Habari Mseto

Kibarua adungwa kisu alipofumaniwa na mke wa mtu kitandani

July 22nd, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

MAISHA ya kibarua mmoja katika Kaunti ya Kirinyaga yako hatarini baada ya kudungwa kwa kisu na mwanamume ambaye alimpata kitandani na mkewe.

Inadaiwa kuwa mume huyo alikuwa ameondoka nyumbani kuelekea kazini Jumatatu asubuhi, lakini akagundua alikuwa amesahau kitambulisho.

Hata hivyo, aliporejea nyumbani alishangaa kumpata mfanyakazi huyo kitandani na mkewe, ndipo akapandwa na hasira na kuchukua kisu, akamdunga mikononi na sehemu nyingine za mwili, akimsababishia majeraha tele mwilini.

Kisa hicho kilitokea katika kituo cha kibiashara cha Mutithi.

Mshukiwa alipiga mayowe akitafuta usaidizi, nduru zake zikiwavutia wakazi wengi ambao walimwokoa na kumkimbiza katika hospitali ya kibinafsi ya White Rose, ambapo bado anatibiwa baada ya kushonwa majeraha.

Mume husika alikamatwa na polisi wa utawala eneo hilo na bado anazuiliwa akihojiwa, wakazi wakisema alikuwa karibu kumuua mfanyakazi huyo.

“Ikiwa wakazi wasingefika kwa haraka na kuingilia kati, angemuua mwathiriwa,” akasema Bi Caroline Wambui, mkazi.

Wakazi walisema kuwa wakati hali bado ilikuwa tete mshukiwa na mfanyakazi huyo wakikabiliana, mwanamke husika alitoroka na kuenda pasipojulikana.

“Alitoroka kutoka ndani ya nyumba na kumuacha mumewe akimvamia mfanyakazi huyo,” Bi Wambui akasema. Bw John Mwangi, jirani mwingine alisema kuwa alikuwa nyumbani wakati huo ndipo akasikia kemi kutoka kwa mwathiriwa, akisema alipofika alimpata akigaagaa chini kwa uchungu.