Kibarua cha Gor Mahia kukabiliana na mikosi ya ugenini soka ya CAF baada ya kichapo kutoka kwa Napsa

Kibarua cha Gor Mahia kukabiliana na mikosi ya ugenini soka ya CAF baada ya kichapo kutoka kwa Napsa

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia watahitaji kufuta mikosi ya muda mrefu kusalia katika Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederation Cup) baada ya kulemewa 1-0 na wageni wao NAPSA Stars katika mechi ya kuingia makundi, Jumapili.

Gor, ambayo sasa haina ushindi katika mechi 12 mfululizo za ugenini katika mashindano yote ya Afrika, ilizamishwa na bao la Daniel Adoko.

Beki huyo wa Ghana mwenye umri wa miaka 21 alitikisa nyavu za K’Ogalo dakika ya 86. Timu hizo zilikuwa zinakutana kwa mara ya kwanza kabisa.

Rekodi ya Gor mbali na ardhi yake ni ya kusikitisha. Katika mechi 12 za mwisho wamecheza ugenini kati ya Desemba 16 mwaka 2018 na Februari 14, 2020 kwenye Klabu Bingwa Ulaya ama Kombe la Mashirikisho, Gor haina ushindi. Imepoteza dhidi ya CR Belouizdad 6-0 (Algeria), APR 2-1 (Rwanda), DC Motema Pembe 2-1 (DR Congo), Berkane 5-1 (Morocco), Zamalek 4-0 (Misri), NA Hussein Dey 1-0 (Algeria), Petro de Luanda 2-1 (Angola), Lobi Stars 2-0 (Nigeria), Big Bullets 1-0 (Malawi) na USM Alger 2-1 (Algeria) na kutoka 0-0 dhidi ya Aigle Noir (Burundi) na New Star (Cameroon).

Mechi ya mwisho ambayo Gor ilishinda ugenini ilikuwa dhidi ya Young Africans (Yanga) kutoka Tanzania 3-2 Julai 29, 2018.

Takwimu hizo zinatoa picha kuwa Gor ya kocha Vaz Pinto itahitaji kusakata kabumbu ambayo haijacheza kwa muda mrefu ili kuokoa kampeni yake inayoning’inia pabaya.

Ikifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ua marudiano Februari 21 dhidi ya NAPSA ambayo imeajiri Wakenya David Owino ‘Calabar’ (beki) na Shaaban Odhoji (kipa), Gor itaingia mduara wa kupokea tuzo ya kifedha kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Droo ya mechi za makundi itafanywa Februari 20.

You can share this post!

Siasa za matusi ni hatari – Mukhisa Kituyi

Wezi wavamia makazi ya meya wa zamani wa Thika