Kibarua cha IEBC kuandaa duru ya pili ya uchaguzi 2022

Kibarua cha IEBC kuandaa duru ya pili ya uchaguzi 2022

Na WANDERI KAMAU

KENYA inakabiliwa na kibarua cha maandalizi ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais, ikiwa itajipata hapo kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kulingana na wadadisi wa siasa, kuna uwezekano mkubwa Kenya kujipata hapo, ikizingatiwa huenda kusipatikane mshindi wa moja kwa moja kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo.

Huo utakuwa uchaguzi wa tatu kufanywa chini ya Katiba ya 2010 nchini, baada ya chaguzi kuu za 2013 na 2017.Kulingana na Katiba, lazima mwaniaji anayetangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa urais kupata asilimia 50+1 ya kura.

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa, kibarua kikuu kinachoziandama taasisi muhimu kama Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni kuhusu mikakati ambayo imeweka kama matayarisho ya hali hiyo.

“Lazima taasisi kama IEBC ijitokeze wazi kuwaelezea Wakenya na wadau wengine muhimu kuhusu juhudi ilizoweka kuona kuwa imejitayarisha kuandaa duru ya pili ya uchaguzi wa urais, ikiwa hilo litatokea,” asema Bw Felix Otieno, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya chaguzi.

Ingawa hadi sasa si wazi kuhusu idadi kamili ya watu ambao watajitokeza kuwania urais, ushindani mkuu unatabiriwa kuwa kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumanne, Dkt Ruto alitangaza kuwa huenda chama cha UDA kisibuni muungano wowote wa kisiasa na vyama vingine, akieleza wanalenga kukikuza chama kuwa cha kitaifa.

“Tumeona jinsi miungano ya kisiasa hugeuka kuwa majukwaa ya usaliti na udhalilishaji wakati inapovunjika. Ili kuepuka tatizo hilo, tunataka kujenga na kukuza chama chetu (UDA) kuwa cha kitaifa. Hili ni kinyume na siasa za awali, ambapo miungano ya kisiasa huwa imekitwa katika ukabila,” akasema Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuwa katika hali ambapo ushindani wa kisiasa utakuwa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga, huenda kusipatikane mshindi wa moja kwa moja.

“Hawa ni viongozi wawili wenye umaarufu karibu sawa kote nchini. Ni vigogo wanaoungwa mkono katika karibu kila pembe ya nchi. Bila shaka, hilo linamaanisha yule atakayeibuka mshindi atamshinda mwenzake kwa asilimia ndogo tu ya kura. Vivyo hivyo, yule atakayeshindwa, atashindwa kwa pengo ndogo sana,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanasema, ikizingatiwa kwa mujibu wa katiba ya sasa lazima kuwe na mshindi wa moja kwa moja, sharti wadau na taasisi husika kuhakikisha juhudi zote zimechukuliwa kuona Kenya haitajipata katika kizungumkuti cha kisiasa kama 2007.

Vile vile, wanafananisha hilo na 2017, ambapo ilimlazimu Rais Uhuru Kenyatta kubuni handisheki na Bw Odinga, kwani alikuwa akiidhibiti nusu moja ya nchi.

“Kuna hatari kubwa ikiwa IEBC na taasisi nyingine hazijajitayarisha kwa uwezekano ambapo Kenya itajipata kwenye duru ya pili ya uchaguzi.

“Sababu kuu ni kuwa kama ilivyoshuhudiwa katika miaka ya 2007 na 2017, huenda ikawa vigumu kwa kiongozi anayechaguliwa kuwa rais kuiendesha serikali, kwani atakuwa tu anaiongoza nusu moja ya nchi.

“Hivyo, itamlazimu kubuni mwafaka wa kisiasa na yule atakayeibuka wa pili kwenye uchaguzi huo, kwani kama yeye, atakuwa anaidhibiti nusu nyingine ya nchi,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Mdadisi huyo anaeleza kuwa taswira hiyo ndiyo iliyowalazimu Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Rais Kenyatta kubuni ushirikiano wa kisiasa na Bw Odinga, kwani licha ya kushindwa kwenye chaguzi hizo, bado alikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakimfuata.

“Tofauti ya ushindi wa Bw Kibaki na Bw Odinga mnamo 2007 ilikuwa ndogo sana, kiasi kwamba baadhi ya wafuasi Bw Odinga waliamini ndiye aliyeibuka mshindi. Vivyo hivyo, mnamo 2017, wafuasi wa Bw Odinga waliamini serikali ilimwibia kura zake, kwani ni kiongozi mwenye ushawishi na ufuasi mkubwa,” asema Bw Muga.

Hata hivyo, anasema hali hizo zingeweza kuepukwa, ikiwa kungekuwa na taasisi muhimu na zinazoaminika na wananchi, kama vile IEBC, Idara ya Mahakama, Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) na Idara ya Polisi.

“Mnamo 2007, Bw Odinga alisema hangeenda mahakamani kwani aliamini hangepata haki. Ni sababu hiyo ambapo aliiomba jamii ya kitaifa kuingilia kati ili kuisaidia Kenya. Vivyo hivyo, kutoaminika kwa Idara ya Mahakama mnamo 2017 ndiko kulikochangia ghasia ambazo zilitokea. Haya yalichangiwa na ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa taasisi muhimu,” asema Bw Muga.

Kwa hayo, wadadisi wanaeleza imefikia wakati wakuu wa idara hizo kuanza kuonyesha ushirikiano wa pamoja miongoni mwa Wakenya ili kujenga imani yao tunapoelekea 2022.

Licha ya hofu hizo, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati anasema wamejitayarisha kukabili hali yoyote itakayotokea, hasa baada ya Rais Kenyatta kuidhinisha majina ya watu wanne watakaojaza nafasi ambazo zimekuwa wazi katika tume hiyo.

You can share this post!

Shambulizi la bomu 1998 lilivyomtosa kwa usanii

Siasa za urithi wa Ongwae zachukua mkondo wa ukoo