Makala

Kibarua cha kukabiliana na janga la ulevi Mlima Kenya

February 11th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

VIFO vya zaidi ya watu 10 katika Kaunti ya Kirinyaga wiki jana kutokana na pombe haramu, vimeibua kumbukumbu kuhusu vita ambavyo viongozi tofauti wamekuwa wakiendesha katika eneo la Mlima Kenya kukabiliana na ulevi.

Ingawa Naibu Rais Rigathi Gachagua ametangaza vita vikali dhidi ya wauzaji wa pombe hizo, yeye si kiongozi wa kwanza kuendesha juhudi hizo bila mafanikio.

Viongozi wengine waliowahi kuendesha vita hivyo ni Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, aliyekuwa mbunge wa Naivasha John Mututho na aliyekuwa gavana wa Kaunti ya Kiambu, Bw Ferdinand Waititu.

Mnamo 2010, Bw Mututho aliibukia kuwa kiongozi wa kwanza wa kisiasa kujitokeza hadharani, na kutangaza kwamba mustakabali wa Mlima Kenya ulikuwa hatarini kutokana na ongezeko la ulevi, hasa miongoni mwa vijana.

Kutokana na visa vya makumi ya watu waliokuwa wakifariki kutokana na unywaji wa pombe haramu, mbunge huyo aliwasilisha mswada bungeni, ulioibukia kuitwa ‘Sheria ya Mututho’.

Lengo kuu la sheria hiyo lilikuwa ni kudhibiti wakati ambapo pombe inafaa kuuzwa.

Sheria hiyo pia inaeleza kuwa wauzaji pombe wanafaa kuwa na leseni halali kutoka kwa idara husika, ili kuhakikisha kuwa pombe inayouzwa kwa umma ni salama.

Licha ya Bunge la Kitaifa kupitisha mswada huo na kuwa sheria, Bw Mututho anasema kuwa kumekuwa na ulegevu mkubwa kwenye utekelezaji wake.

“Naunga mkono juhudi zinazoendeshwa, japo lazima ziandamane na utekelezaji wa Sheria ya Mututho kuhusu vita dhidi ya uuzaji pombe haramu,” akasema majuzi.

Kando na Bw Mututho, Bw Kenyatta pia alijaribu kukabiliana na janga hilo mnamo Juni 2015.

Mwaka huo, Bw Kenyatta alikutana na wabunge wote kutoka ukanda wa Mlima Kenya katika Ikulu, ambapo aliwaagiza kuhakikisha wanashirikiana ifaavyo maafisa wa utawala kutoka maeneobunge yao ili kumaliza uuzaji wa pombe hizo.

Kikao hicho kilifanyika baada ya karibu watu 20 kufariki mwezi uliotangulia katika eneo la Kati, baada ya kunywa pombe haramu.

Wengine walipofuka.

“Nawaagiza mrejee katika maeneobunge yenu na kuhakikisha kuwa mmeshirikiana ifaavyo na maafisa wa utawala kukabiliana na uuzaji wa vileo haramu. Lazima mtindo huu ukome. Hatutawapoteza watu wetu tena,” akafoka Bw Kenyatta.

Juhudi hizo pia ziliendeshwa na Bw Waititu, alipohudumu kama gavana wa Kiambu na mbunge wa eneo la Kabete.

Akiwa gavana, Bw Waititu alianza mpango ulioitwa ‘Kaa Sober’, ambao lengo lake kuu lilikuwa ni kupunguza visa vya wanaume kujiingiza katika visa vya ulevi, na badala yake kufanya kazi au vibarua.

Chini ya mpango huo, wanaume na vijana waliokuwa wakishiriki kwenye kazi hizo walikuwa wakilipwa na kaunti.

Hata hivyo, mpango huo ulisimamishwa baada ya kukumbwa na madai ya ufisadi. Pia, ilidaiwa kuwa watu waliolipwa pesa hizo walirejea ulevini kununua pombe.

Kutokana na hayo, wadadisi wanasema kuwa ili kushinda vita hivyo, Bw Gachagua “atahitaji kujitolea kwa njia ya kipekee”.

“Hivi ni vita vinavyohitaji juhudi za kipekee,” asema Bw Martin Mwangi, ambaye ni mkazi wa Kaunti ya Nyandarua.