Siasa

Kibarua cha kuokoa UhuRuto

October 15th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

JUHUDI za viongozi wa kidini za kupatanisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, huenda zikakumbwa na vizingiti kutokana na misimamo ya wawili hao kuhusu masuala yaliyowatenganisha.

Wadadisi wa kisiasa wanasema Rais Kenyatta yuko njia panda kwa sababu ya ushirika wake wa kisiasa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambao Dkt Ruto hajakumbatia.

Dkt Ruto amekuwa akisema Bw Odinga anatumia handisheki kuvunja chama cha Jubilee ili kumzuia asikitumie kugombea urais 2022.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta amekuwa akimtetea Bw Odinga akisema lengo la ushirikiano wao ni kuunganisha nchi na kupigana na ufisadi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), ambao Dkt Ruto amekosoa vikali.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, kuridhiana na Dkt Ruto kunaweza kuvunja handisheki, jambo ambalo linaweza pia kulemaza BBI.

Kulingana na mdadisi wa siasa Tom Maosa, itabidi Rais Kenyatta asawazishe kati ya maslahi ya Dkt Ruto na mipango yake na Bw Odinga.

“Kuna kizingiti kwa upande wa Rais kwa sababu kuridhiana na Dkt Ruto kunaweza kuhatarisha uhusiano wake na Bw Odinga na mpango mzima wa BBI. Kwa maoni yangu, anaweza kuvuka kizingiti hiki kwa kuhakikisha mazungumzo ya kupatana na Dkt Ruto yanahusu kufanikisha mchakato huo,” asema.

Wachanganuzi wanasema ikizingatiwa uhasama kati ya viongozi hao wawili umejikita katika chama tawala cha Jubilee na serikalini, kuna uwezekano wa wandani wa Rais na washauri wake kutochangamkia juhudi za kuwapatanisha, hasa miongoni mwa maafisa wakuu wa chama wa Jubilee na wa serikali, wakiwemo mawaziri ambao wamekuwa wakimdharau Dkt Ruto hadharani.

Baadhi yao wametumia kutengwa kwa Dkt Ruto serikalini kujipendekeza kwa Rais. Miezi miwili iliyopita, Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko alidai Dkt Ruto ni karani tu na hafai kumkaidi Rais. Naye waziri wa Usalama Fred Matiang’i amekuwa mstari wa mbele kumhujumu Dkt Ruto kwa kutumia polisi kuvunja mikutano yake.

Naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe amewahi kuapa kwamba Dkt Ruto hatakuwa rais, naye Katibu Mkuu wa chama hicho Raphael Tuju majuzi alimkemea akidai amekwepa majukumu yake.

“Hawa ni watu wa karibu sana na Rais ambao kwa njia moja au nyingine wamenufaika na uhusiano baridi kati ya viongozi hao wawili. Ikizingatiwa baadhi yao ni wandani wa Rais na wana maslahi ya kulinda, huenda wakawa kizingiti kwa juhudi za upatanishi zinazoendeshwa na viongozi wa kidini,” asema mchanganuzi wa masuala ya siasa, Benard Kamau.

Anasema Rais Kenyatta ana kibarua kwa sababu ya matakwa ya Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa ambao wanaweza kutumia juhudi hizo kushinikiza avunje uhusiano wake na Bw Odinga: “Akifanya hivyo, huu utakuwa mwisho wa BBI ambayo ameunga mkono.”

Mdadisi huyo anasema hii inaweza kurejesha nchi ilipokuwa imegawanyika kabla ya handisheki,” asema.

Hii inaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi ikizingatiwa kuwa wafadhili wa kimataifa wameanza kuwa na wasiwasi kuhusu migawanyiko ya kisiasa nchini miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu.

Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini, Kabando wa Kabando, anasema Rais Kenyatta yuko katika njia panda: “Kuna uwezekano wa Uhuruto kufufuka lakini ili Rais Kenyatta kujikwamua, suluhisho ni kuachana na BBI na kuelekeza juhudi zake kufufua uchumi. Ruto hawezi kuzimwa, na Odinga hawezi kuthibitiwa,” Bw Kabando asema.

Katika hatua ya kuonyesha anayopitia Rais kwa wakati huu, washirika wa Dkt Ruto walishabikia juhudi za viongozi wa kidini.

“Sasa uchumi utakuwa thabiti kupitia handisheki ya nguvu ambayo itatangazwa hivi karibuni kati ya Uhuru na Ruto,” alisema Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.