Kibarua cha Raila na Uhuru kutetea Cherera na wenzake

Kibarua cha Raila na Uhuru kutetea Cherera na wenzake

NA BENSON MATHEKA

VIGOGO wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga na Uhuru Kenyatta, wana kibarua cha kuwatetea makamishna wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wanaolengwa kutimuliwa ofisini na muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, Jumanne alisema amepokea maombi manne ya kutaka kutimua makamishna hao waliojitenga na Mwenyekiti wa Tume Wafula Chebukati, kwa kumtangaza Rais William Ruto mshindi wa uchaguzi wa urais wa Agosti 9.

Makamishna hao naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit, Justus Nyang’aya na Francis Wanderi sasa wanasubiri hatima yao baada ya maombi ya kuwatimua kuwasilishwa Bungeni.

Wabunge wa Kenya Kwanza wamekuwa wakitisha kuwatimua makamishna hao wakidai walikiuka maadili ya kazi yao na hawafai kuendelea kuhudumu katika tume.

Hata hivyo, viongozi wa Azimio wakiongozwa na Bw Odinga na Uhuru Kenyatta (mwenyekiti wa muungano wa upinzani) wamekuwa wakiwatetea wanne hao huku kiongozi wa ODM akisema kwamba watawalinda.

Baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wa Rais Ruto, Uhuru, aliyekuwa mamlakani wakati huo, alionekana kuunga makamishna hao kwa kushangaa kwa nini majaji walifumbia macho ukweli kwamba wengi wa makamisha walijitenga na matokeo.

Huku duru zikisema kwamba Rais Ruto aliwapa wabunge wa Kenya Kwanza idhini ya kuwatimua makamishna hao na ikizingatiwa kwamba muungano huo tawala una idadi kubwa ya wabunge, inasubiriwa kuona hatua ambazo Bw Odinga na Uhuru watachukua kuwatetea na kuwalinda makamishna hao.

“Kuna mchakato mrefu wa kuwatimua makamishna wa IEBC na una gharama zake lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba mwishowe, makamishna hao wataondolewa ofisini iwapo Kenya Kwanza, hasa kinara wake Rais Ruto hatabadilisha nia,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Anataja matamshi ya Bw Odinga na Azimio kwamba watawatetea makamishna hao kama yasiyo na nguvu.

“Azimio hawana nguvu katika Bunge la Taifa ikilinganishwa na Kenya Kwanza ambao wako na wabunge wengi na serikali,” asema.

Hata hivyo, anasema wanachoweza kufanya vinara hao wa upinzani ni kwenda kortini au kuwafadhili makamishna hao kwenda kortini baada ya mchakato wa kisheria wa kuwatimua.

Wakili wa masuala ya Kikatiba Bob Mkangi anasema mchakato wa kuwatimua makamishna hao unahitaji wapatiwe nafasi ya kujitetea kwa madai dhidi yao.

Juhudi za kuwatimua makamishna zimeanza kushika kasi huku muhula wa Bw Chebukati na makamishna wawili waliokuwa upande wake Boya Molu na Profesa Abdi Guliye ukikamilika.

Watatu hao wanapaswa kuondoka katika tume huyo kufikia Januari 23, 2023.

Duru zinasema kuwa juhudi za kutimua Cherera na kundi lake zinaendelea wakati tofauti zimechacha katika IEBC, wanne hao wakitengwa katika shughuli za tume ikiwemo maandalizi ya chaguzi ndogo zijazo.

  • Tags

You can share this post!

Mbwa waelekeza wakazi ulikozikwa mwili katika kijiji cha...

CECIL ODONGO: Wanasiasa Nyanza wanaosaka kazi serikalini...

T L