Na RUTH MBULA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na kibarua kikubwa katika Kaunti ya Kisii, huku wagombeaji wa viti mbalimbali waking’ang’ania tiketi ya chama hicho.
Hii ni kutokana na idadi kubwa ya wanasiasa ambao waligura ODM kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 ambao wamerejea katika chama hicho.
Kwa mfano, mnamo Alhamisi wiki jana, Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Richard Onyonka, aliyekuwa Mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Kisii Samuel Omwando, wabunge wa zamani Simon Ogari na Robert Monsa, walirejea katika chama cha ODM.
Bw Onyonka aligura chama cha Ford Kenya huku Bw Omwando akihama chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto.
Wanasiasa hawa waliokuwa miongoni mwa kundi la zaidi ya wanasiasa 50 kutoka Kaunti ya Kisii walipokewa na Bw Odinga katika makao makuu, Jumba la Orange, Nairobi.
Viongozi wote wa ODM katika kaunti hiyo, hawakuhudhuria shughuli hiyo huku duru zikisema kuwa hawakufurahia hatua ya wanachama hao “waasi” kurejea kushindana nao.
Vile vile, tangazo la Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati kwamba atawania kiti cha ugavana wa Kisii limeongeza joto la kisiasa katika Kaunti ya Kisii.
Bw Arati ambaye ni mwandani wa Bw Odinga ndiye aliwapeleka wanasiasa waliojiunga na ODM kwa kiongozi huyo wa chama, katika majawapo ya mikakati yake ya kudhibiti chama hicho katika kaunti.
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Bw Arati ameendesha kampeni kali dhidi ya uongozi wa ODM katika kaunti ya Kisii ukiongozwa na Gavana James Ongwae, Seneta Sam Ongeri na Mbunge Mwakilishi Janet Ong’era.
Kundi la wanasiasa waliojiunga upya na ODM, sasa linaungana na wagombeaji wengine ambao wamekuwa waaminifu kwa chama kusaka tiketi ya chama hicho, hatua ambayo itamkosesha usingizi Bw Odinga.
“Leo tumepokea wanasiasa kadha waliogura vyama vya na kujiunga na ODM. Waliongozwa na Bw Onyonka, wabunge wa zamani Simon Ogari na Dkt Monda. Zaidi ya wanasiasa 50 wakiwemo viongozi wa vijana katika UDA wamejiunga na ODM,” ODM ikasema kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Bw Onyonka alifichua kuwa amejiondoa kutoka wadhifa wake wa Naibu Kiongozi wa Ford Kenya kutokana na mkanganyiko wa kimasilahi.
“Mimi sio kiongozi wa Ford Kenya. Nilijiondoa majuma mawili yaliyopita chama kilipoandaa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wake (NDC). Singeendelea kukaa ndani ya Ford Kenya ikiwa ukweli ni kwamba namhusudu Raila,” akasema mbunge huyo ambaye anahudumu muhula wake wa tatu bungeni.
Bw Arati tayari amelalamikia baadhi ya mbinu ambazo huenda zikakumbatiwa na ODM wakati wa uteuzi wa chama, akisema zitawafungia nje wawaniaji maarufu na kuchangia chama kupoteza nyadhifa mbalimbali.
Alidai kuwa kuna baadhi ya wanasiasa ambao watatumia ushawishi wao kuwapendelea viongozi mbalimbali.
Aidha Bw Arati, alisema wawaniaji ambao watahisi wamedhulumiwa na ODM, wataghairi nia na kuhamia vyama vingine au kusimama kama wawaniaji wenza huku chama kikisalia dhaifu.
“Haya ndiyo mambo ambayo yamekuwa yakifanyika kwa miaka mingi. Huenda tutakuwa tukirudia makosa ya hapo awali na hili litatuponza sana. ODM inafaa iandae mchujo ambao utakuwa huru na haki,” akasema Bw Arati.
Bw Arati ambaye amekuwa akiendesha kampeni kali atalazimika kupambana na Seneta Ongeri, Bi Ong’era na Naibu Gavana Joash Maangi kwenye mchujo wa ODM.