Michezo

Kibarua kigumu chasubiri Shujaa raga ya Singapore Sevens ikitafuta kujinasua maeneo hatari

April 12th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Shujaa ya kocha Paul Murunga itakuwa mawindoni kupata matokeo mazuri iliyoyapata nchini Singapore mwaka 2016, 2017 na 2018 itakapokutana na Uingereza, Marekani na Wales katika mechi za Kundi C za duru hii ya nane ya Raga ya Dunia mnamo Jumamosi.

Vijana wa Murunga walishinda taji la mwaka 2016 kwa kushangaza Fiji 30-7 katika fainali ya Singapore Sevens mwaka 2016 na kumaliza katika nafasi ya saba mwaka 2017 na tena 2018.

Msimu huu wa 2018-2019, Shujaa inakabiliwa na hatari ya kutemwa kutoka Raga ya Dunia baada ya kusikitisha katika duru saba zilizopita ambazo haikufika hata robo-fainali moja kuu. Inashikilia nafasi ya 13 kwa alama 23, mbili mbele ya nambari 14 Japan na tatu mbele ya Wales inayoshikilia nafasi ya 15. Timu itakayomaliza duru zote 10 katika nafasi ya 15 itatemwa.

Kenya imewahi kukutana na Uingereza na Marekani mjini Singapore. Ina rekodi mbaya sana dhidi ya Uingereza. Ilipepetwa 24-7 mwaka 2005, ikalimwa 26-12 mwaka 2006, ikacharazwa 13-12 mwaka 2017 na kulemewa 28-19 mwaka 2018 na Waingereza. Isipokuwa mwaka 2017, mechi zingine zote dhidi ya Uingereza zimekuwa katika mechi ya makundi.

Kenya ilikutana na Uingereza katika robo-fainali ya Singapore mwaka 2017 na kupoteza 13-12 kabla ya kumaliza ya saba baada ya kuchapwa 24-21 na New Zealand katika nusu-fainali ya kuorodhesha nambari tano hadi nane.

Kocha Paul Murunga wa timu ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya katika hii picha ya awali. Picha/ Chris Omollo

Tangu Kenya ikutane na Uingereza mara ya kwanza mwaka 2004 kwenye raga hii, Uingereza inajivunia rekodi nzuri dhidi ya Waafrika hawa ya ushindi 36, sare nne na kupoteza mara nane pekee. Wakenya wamewahi kukutana na Marekani ya Mike Friday mara moja pekee mjini Singapore. Walilemea Waamerika 33-14 katika mechi hiyo ya makundi mwaka 2018. Wakenya wana rekodi nzuri dhidi ya Waamerika ya ushindi 23 dhidi ya 16, huku wakitoka sare mara tatu kwenye Raga ya Dunia.

Shujaa italazimika kujikakamua katika kundi hili ili kufika robo-fainali kuu kwa sababu mbali na kuwa na rekodi mbovu dhidi ya Uingereza, Wales pia huwa mwiba kwake. Ingawa mataifa haya hayajawahi kukutana mjini Singapore, Kenya imechapwa mara 22 na Wales dhidi ya 18. Mataifa haya mawili hayajawahi kutoka sare.

Baadhi ya wachezaji Kenya itatumai watamka vyema kuongoza kampeni yake ya kujiondoa katika maeneo ya kushushwa ngazi ni Andrew Amonde, Nelson Oyoo na Daniel Sikuta pamoja na nahodha Jeffrey Oluoch. Ili kufaulu katika kampeni yake, italazimika kutumia nafasi zake vyema na kuimarisha ulinzi katika ngome yake. Pia, lazima iwe macho na wachezaji matata Waingereza Dan Norton, Michael Ellery na Richard de Carpentier, Waamerika Carlin Isles, Stephen Tomasin na Martion Iosefo na raia wa Wales Ethan DaviesTomi Lewis na Tom Rodgers.

 

Ratiba (Aprili 13, 2019):

Kundi A

Afrika Kusini na Scotland (7.14am)

Fiji na Canada (7.36am)

Afrika Kusini na Canada (10.40am)

Fiji na Scotland (11.02am)

Scotland na Canada (2.06pm)

Fiji na Afrika Kusini (2.28pm)

Kundi B

Argentina na Australia (6.30am)

Ufaransa na Hong Kong (6.52am)

Argentina na Hong Kong (9.56am)

Ufaransa na Australia (10.18am)

Australia na Hong Kong (1.22pm)

Ufaransa na Argentina (1.44pm)

Kundi C

Uingereza na Kenya (5.44am)

Marekani na Wales (6.06am)

Uingereza na Wales (9.12am)

Marekani na Kenya (9.34am)

Kenya na Wales (12.38pm)

Marekani na Uingereza (1.00pm)

Kundi D

New Zealand na Japan (5.00am)

Samoa na Uhispania (5.22)

New Zealand na Uhispania (8.28am)

Samoa na Japan (8.50am)

Japan na Uhispania (11.54am)

Samoa na New Zealand (12.16pm)