Michezo

Kibarua kigumu kwa Barcelona na Chelsea katika raundi ya 16-bora UEFA

December 14th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

NYOTA Lionel Messi na Neymar Jr huenda wakakutana tena katika uwanja mmoja wa soka – mara hii kila mmoja akicheza dhidi ya mwenzake – baada ya Barcelona kutiwa katika zizi moja na Paris Saint-Germain (PSG) kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Gozi hilo linatarajiwa kuwa la kusisimua zaidi kwenye hatua hiyo ya mwondoano baada ya droo ya 16-bora kufanyika mnamo Disemba 14, 2020 jijini Nyon, Uswisi.

Mechi hizo za mikondo miwili kati ya Barcelona na PSG zitarejesha kumbukumbu za 2017 ambapo PSG walikung’uta Barcelona 4-0 katika mkondo wa kwanza jijini Paris kabla ya Barcelona kulipiza kisasi na kuwabandua miamba hao wa Ufaransa kwa ushindi mnono wa 6-1 kwenye marudiano yaliyofanyika nchini Uhispania.

Kwingineko, klabu zote tatu za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zimepangiwa kuanza kampeni zao za hatua ya 16-bora ugenini kabla ya kuchuma nafuu kwenye marudiano yatakayoandaliwa katika viwanja vyao vya nyumbani.

Manchester United waliokuwa wakirejea kunogesha kivumbi cha UEFA msimu huu kwa mara ya kwanza tangu 2017 walibanduliwa mapema kwenye hatua ya makundi na kushuka hadi Europa League baada ya kuzidiwa maarifa na PSG na Leipzig kwenye Kundi H lililojumuisha pia Istanbul Basaksehir ya Uturuki.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool ambao walitawazwa wafalme wa UEFA mnamo 2018-19, watapepetana na RB Leipzig ya Ujerumani huku Manchester City ya mkufunzi Pep Guardiola ikichuana na Borussia Monchengladbach ambayo pia inashiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Monchengladbach wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya soka ya UEFA kwa mara ya kwanza tangu 1978.

Chelsea wanaotiwa makali na kocha Frank Lampard watakuwa pia na kibarua kizito dhidi ya Atletico Madrid ambao kwa sasa wanajivunia fomu nzuri katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) chini ya mkufunzi raia wa Argentina, Diego Simeone.

Mabingwa watetezi Bayern Munich kutoka Ujerumani wamepangwa kuvaana na Lazio inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Ni mara ya kwanza tangu mwaka wa 2000 kwa Lazio kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA.

Mnamo 2019-20, kocha Hansi Flick aliwaongoza Bayern kuwadhalilisha Barcelona 8-2 kwenye robo-fainali ya UEFA kabla ya kuwapokeza PSG kichapo cha 1-0 hatimaye kwenye fainali na kutwaa ubingwa wa taji hilo jijini Lisbon, Ureno.

Miamba wa soka ya Ureno, FC Porto watakwaruzana na Juventus ambao ni wapambe wa kabumbu kutoka Italia. Sevilla waliotawazwa mabingwa wa Europa League mnamo 2019-20 chini ya kocha Julen Lopetegui watapepetana na Borussia Dortmund ya Ujerumani huku mabingwa mara 13 wa UEFA, Real Madrid wakikwaruzana na Atalanta kutoka Italia.

Mechi za mkondo wa kwanza katika raundi hiyo ya 16-bora zitatandazwa kati ya Februari 16-24, 2020 huku marudiano yakiandaliwa kati ya Machi 9-19. Droo ya hatua ya robo-fainali na nusu-fainali itafanyika Machi 19.

DROO YA 16-BORA UEFA:

Monchengladbach na Man-City

Lazio na Bayern Munich

Atletico Madrid na Chelsea

FC Porto na Juventus

RB Leipzig na Liverpool

Barcelona na PSG

Sevilla na Borussia Dortmund

Atalanta na Real Madrid