Michezo

Kibarua kinachosubiri Kamworor katika Nusu-Marathon Duniani 2020

September 24th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mara tatu wa Nusu-Marathon Duniani Geoffrey Kamworor atakabiliwa na ushindani mkali katika kutetea taji lake katika makala ya mwaka 2020 yatakayofanyika mjini Gdynia nchini Poland mnamo Oktoba 17.

Hii ni baada ya Uganda kutangaza kikosi kikali kitakachowania taji hilo ambalo nchi hiyo haijawahi kushinda katika historia yake.

Orodha ya Uganda inajumuisha bingwa wa dunia wa mbio za mita 10,000 Joshua Cheptegei, ambaye amekuwa akitetemesha kwa miezi kadha katika kila umbali wa mbio ameshiriki.

Cheptegei, ambaye pia ni bingwa wa dunia wa mbio za nyika, alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 5,000 mjini Monaco mwezi uliopita. Timu ya Uganda pia ina mtimkaji Jacob Kiplimo, ambaye alitesa majuzi kwenye Riadha za Dunia za Continetal Tour katika kitengo cha mbio za mita 5,000 mjini Ostrava nchini Jamhuri ya Czech .

Kiplimo pia aliweka muda bora duniani mwaka 2020 katika mbio za mita 3,000 alipokamilisha duru ya Diamond League ya Roma nchini Italia kwa dakika 7:26.64, ambayo ni rekodi ya kitaifa nchini mwake na ni mkimbiaji wa kwanza aliye chini ya umri wa miaka 20 kukamilisha umbali huo kwa kasi hiyo.

Mbali na wakali hao wawili, Kamworor pia atakutana uso kwa macho na Stephen Kissa na Abel Chebet wanaokamilisha orodha ya wawakilishi wa Uganda katika kitengo cha wanaume.

Rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya wanaume inashikiliwa na Kamworor aliyetimka Copenhagen Half Marathon kwa dakika 58:01 mnamo Septemba 2019.

Uganda itawakilishwa na Juliet Chekwel, Doreen Chemutai, Doreen Chesang na Rachael Zena Chebet katika kitengo cha kinadada ambacho Kenya ilishinda mara ya mwisho kupitia Peres Jepchirchir mwaka 2016. Jepchirchir alivunja rekodi ya dunia ya mbio hizi za kilomita 21 alipotimka umbali huo kwa saa 1:05:34 mjini Prague nchini Czech mnamo Septemba 5.

Timu ya Kenya iliyotajwa Machi 2020 kwa mashindano haya ilijumuisha Leonard Barsoton, Victor Kimutai Chumo, Geoffrey Kamworor, Kibiwott Kandie, Shadrack Kimining Korir (wanaume) na Dorcas Jepchirchir, Pauline Kamulu, Dorcas Kimeli, Brillian Jepkorir Kipkoech na Monica Wanjuhi (wanawake). Huenda timu hii ikafanyiwa mabadiliko.

Mashindano haya yaliahirishwa kutoka Machi hadi Oktoba kutokana na janga la virusi vya corona.