Michezo

Kibarua kwa Olunga kuonyesha makali yake Japan

August 13th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kutia wino kandarasi ya miaka mitatu inayoandamana na mshara wa Sh15 milioni, kazi ngumu inasubiri mvamizi Michael Olunga katika klabu yake mpya ya Kashiwa Reysol kwenye Ligi Kuu ya Japan (J1 League).

Nambari 13 Reysol itaalika nambari 12 Vegalta uwanjani Hitachi Kashiwa hapo Agosti 11 saa saba mchana katika ligi hii ya klabu 18.

Reysol iliambulia pakavu katika mechi nne ilipopepetwa nyumbani 2-0 na Shonan Bellmare na 1-0 na FC Tokyo na kulimwa ugenini 1-0 na Vissel Kobe anayochezea Mhispania Andres Iniesta na 6-2 dhidi ya Kashima Antlers kati ya Julai 18 na Agosti 1 kabla ya kuzidi Consadole Sapporo nguvu 2-1 Agosti 5.

Mshambuliaji huyu wa Kenya yuko katika klabu ya nne tofauti katika misimu mitatu baada ya Djurgardens IF nchini Uswidi mwaka 2016, Guizhou Zhicheng nchini Uchina (2017) na Girona nchini Uhispania kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Zhicheng kutoka Septemba 1 mwaka 2017.

Baada ya kandarasi yake ya mkopo katika klabu ya Girona kutamatika mwezi Juni mwaka 2018, Olunga alirejea Zhicheng, ambayo imeuzia Reysol.