Kibarua kwa Rais Suluhu joto la kudai katiba mpya likiongezeka

Kibarua kwa Rais Suluhu joto la kudai katiba mpya likiongezeka

Na MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM, Tanzania

UPINZANI nchini Tanzania sasa unadai kuwa viongozi 41 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekamatwa huku shinikizo za kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuanza mchakato wa kuandika katiba mpya zikiendelea kuongezeka.

Makamu kiongozi wa Chadema Tundu Lissu, Jumatatu alidai kwamba familia za viongozi wa upinzani waliotiwa mbaroni zimekatazwa kuwaona jamaa zao.

Miongoni mwa viongozi walio mikononi mwa polisi ni mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe aliyekamatwa mnamo Julai 21 jijini Mwanza alipoenda kuhudhuria kongamano la kudai katiba mpya.

Baadaye Mbowe alifunguliwa mashtaka ya kupanga ugaidi.

Viongozi wa Chadema wanataka kuwepo kwa katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Jumatatu alimtaka Rais Suluhu kueleza Watanzania ni lini anapanga kuanza kuandika katiba mpya na viongozi wa Serikali kutegua kitendawili cha lini mchakato wa mabadiliko ya Katiba utahitimishwa ili Taifa liwe na utulivu.

Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Juni 28, 2021 alisema kuwa hayuko tayari kushughulikia suala la katiba kwani anaendelea na vita dhidi ya ugonjwa wa corona na kuinua uchumi.

“Rasimu ya katiba mpya tayari ipo, kilichosalia ni kukusanya maoni ya wananchi na kisha kuandaaa kura ya maoni,” alisema Jaji Mstaafu Warioba ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kuandaa rasimu ya katiba mpya 2014.

Mchakato wa kuandika katiba mpya nchini Tanzania ulianza 2011 ambapo bunge liliidhinisha sheria ya kutoa mwongozo kuhusu namna ya kuandika katiba mpya.

Mnamo 2013, bunge lilipitisha sheria ya kutoa mwongozo namna ya kuendesha kura ya maamuzi.

Alisema ikiwa haiwezekani kuandaa kura ya maamuzi kubadili katiba mwaka huu wa 2021, Rais Suluhu anafaa kujitokeza na kutangaza ni lini itafanyika ili kupunguza joto la kisiasa.

“Rais ameomba kupewa muda kustawisha uchumi, hilo ni kweli. Lakini anataka muda kiasi kigani? Rais hana budi kueleza nchi ni lini mchakato wa katiba mpya utaendelezwa,” akazema Warioba jijini Dar es Salaam.

Warioba alipendekeze kura ya maamuzi ya kupitisha katiba mpya ifanyike pamoja na uchaguzi wa viongozi wa serikali wa kata na wilaya 2024.

“Rais anaweza kuwaeleza Watanzania wavumilie mpaka 2024 wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, tuunganishe. Wakati wananchi wanapiga kura, wapige na kura ya maamuzi,” akasema.

Warioba alizungumzia umuhimu wa Rais Samia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ili wajadiliane mambo mbalimbali kwa mustakabali wa Taifa, na kwamba bahati nzuri pande zote mbili zimeonyesha utayari katika hilo.

“Ninatarajia kuwa kufikia 2025 tutakuwa na katiba mpya na chama tawala hakitatumia nguvu kuwahangaisha maajenti wa upinzani na kuzuia kiholela baadhi ya wawaniaji kushiriki uchaguzi,” akasema.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikilaumiwa kwa kutumia katiba ya sasa kukandamiza upinzani.

You can share this post!

TAHARIRI: IEBC iwezeshwe kuwasajili wengi

Nyota wa zamani wa Barcelona atua Vissel Kobe ya Japan