Michezo

Kibarua kwa Reading ya Ayub Timbe kuingia EPL

June 22nd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Klabu ya Reading anayochezea Mkenya Ayub Masika Timbe imepata pigo katika juhudi za kuwania tiketi ya kuingia Ligi Kuu baada ya kudondosha alama mbili muhimu katika sare ya 1-1 dhidi ya Stoke. 

Katika mchuano huo, ambao Timbe alitiwa kitini Jumamosi, mshambuliaji Mreno Lucas Joao aliweka Reading kifua mbele dakika ya saba baada ya winga Yakou Meite kutoka Ivory Coast kumpasia mpira safi ndani ya kisanduku uwanjani Madejski.

Nick Powell alinyima Reading ushindi aliposawazisha kutokana na kona sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa.

Reading ni ya 14 kwenye Ligi ya Daraja ya Pili kwa alama 49, nane nje ya mduara wa sita-bora. West Bromwich na Leeds United zinashikilia nafasi mbili za kwanza za kuingia Ligi Kuu moja kwa moja. Nambari tatu hadi sita zitapigania tiketi ya tatu ya kushiriki Ligi Kuu.

Huku Reading ikipata pigo katika kampeni ya kuwania tiketi ya kurejea Ligi Kuu baada ya karibu miaka minane nje, Barnsley anayochezea mzawa wa Kenya Clarke Sydney Omondi Oduor iliduwaza Queens Park Rangers 1-0 uwanjani Loftus Road na kufufua matumaini ya kuepuka kuangukiwa na shoka.

Mshambuliaji Mreno Elliot Simoes alifunga bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya saba. Alipokea mpira kutoka kwa raia wa Wales Ben Williams na kuukamilisha kwa ustadi.

Hull City, Barnsley na Luton Town zinashikilia nafasi tatu za mwisho kwenye ligi hii ya klabu 24 kwa alama 41, 37 na 36 mtawalia. Kabla ya kuchapa nambari 13 QPR, Barnsley ilikuwa ikivuta mkia. Iliruka juu nafasi moja baada ya Luton Town kutoka 1-1 ya Preston.

Zinasalia mechi nane ligi ya daraja ya pili ya msimu wa 2019-2020 itamatike.