Kibarua kwa Ruto kutuliza ulafi bungeni

Kibarua kwa Ruto kutuliza ulafi bungeni

SAMWEL OWINO Na CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto siku ya Alhamisi wiki ijayo atajaribu kutuliza shinikizo za wabunge za kurejeshewa marupurupu yaliyoondolewa na Tume ya Mishahara (SRC).

Dkt Ruto atafika katika majengo ya bunge kutoa hotuba yake ya kwanza kwa kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti kabla ya mabunge hayo kuanza shughuli rasmi.

Hata hivyo, Rais atakuwa akitoa hotuba hiyo siku chache baada ya mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich kuwavunja moyo wabunge kwa kudinda kurejesha marupurupu hayo.

Wabunge wanataka marupurupu yao ya Sh5,000 wanayolipwa kwa kuhudhuria kila kikao, yarejeshwe pamoja na marupurupu ya usafiri.

Lakini katika kikao kilichofanyika katika mkahawa wa Safari Park mnamo Jumatano, Bi Mengich alishikilia kuwa marupurupu ya vikao yamejumuishwa katika mshahara wa Sh710,000 anaolipwa kila mbunge kwa mwezi.

Hata hivyo, ili kutuliza nyoyo za wabunge walioonekana kujawa na hasira, mwenyekiti huyo aliahidi kufanya mkutano na Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ili kujadili matakwa mengine ya wabunge hao.

“Ningependa kuwahakikishia kuwa nimesikia malalamishi yenu. Kwa hivyo, tume yangu itaketi na PSC kujadili masuala hayo kwa lengo la kufikia makubaliano,” Bi Mengich akawaambia wabunge.

Duru za bunge hata hivyo, ziliambia Taifa Leo kuwa huenda SRC ikawasilisha suala hilo kwa Rais Ruto ili aikinge dhidi ya ‘kucha’ za wabunge.

“SRC haitatoa marupurupu ya Sh5,000. Kile ambacho kitafanyika ni kwamba SRC itawasilisha suala hilo kwa Rais ili atoe mwelekeo,” akasema afisa mmoja wa bunge.

Hata hivyo, inasemekana huenda Rais akawaomba wabunge wampe muda kutekeleza ajenda zake kwa raia na matakwa yao yatashughulikiwa kadri muda unavyosonga.

Dkt Ruto atajipata katika hali ngumu kwa sababu anahitaji usaidizi wa bunge kutekeleza ahadi alizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni.

Kwa hivyo, atashughulikia matakwa ya wabunge kwa uangalifu zaidi ili asije akawakasirisha.

Rais Ruto pia atakutana na wabunge hao wanaokabiliwa na hatari ya kupoteza Hazina ya Ustawi wa Maeneo-bunge (NG-CDF) ambayo wamekuwa wakitumia kutekeleza miradi mbalimbali katika maeneo-bunge yao.

Alhamisi, Waziri wa Fedha, Ukur Yatani alisema kuwa Hazina ya Kitaifa haitatoa fedha kwa hazina hiyo (NG-CDF) baada ya Mahakama ya Upeo kuamua kuwa ni haramu.

“Tumepokea agizo la Mahakama ya Upeo kwamba hazina hiyo ilibuniwa kinyume cha Katiba. Kwa hivyo, hatutatoa fedha za NG-CDF hadi pale ambapo tutapata ushauri na mwelekeo kutoka kwa afisi ya Mwanasheria Mkuu,” akasema Bw Yatani, pembezoni mwa mkutano wa hamasisho kwa maseneta mjini Naivasha.

Hata hivyo, wabunge wanashikilia kuwa Mahakama ya Upeo iliharamisha Sheria ya CDF 2013 wala sio sheria ya NG-CDF ya 2015. Wanasema maeneo-bunge yao yataendelea kupokea fedha hizo chini ya sheria ya NG-CDF kwa sababu ndio inatumika wakati huu.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Kuzimwa kwa mawaziri wanaoondoka kutazuia...

GUMZO: Chipukizi Nwaneri aingia mabuku ya Guinness Records

T L