Kibarua sugu chasubiri Shujaa ikielekea mawindoni Seville 7s

Kibarua sugu chasubiri Shujaa ikielekea mawindoni Seville 7s

NA GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga Shujaa iko tayari kupigania matokeo mazuri kwenye duru ya nne ya Raga za Dunia mjini Seville, Uhispania, inayoanza leo baada ya kuteleza Malaga 7s, Uhispania, wikendi iliyopita.

Kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu ameeleza Taifa Spoti katika mahojiano kuwa kikosi hicho kimejiandaa vyema ikiwemo kuchambua video za mechi za Malaga Sevens.

“Timu ina motisha. Tuko tayari kujinyanyua tena,” alitanguliza Namcos katika mahojiano Alhamisi.

“Tumetazama mechi zetu zilizopita na tunaamini kuwa tunaweza kutekeleza kazi yetu vyema wakati muhimu katika mechi,” aliongeza.

Shujaa itaanza kampeni yake mjini Seville saa kumi na moja kasoro dakika 11 leo jioni dhidi ya Australia, iliyomaliza duru tatu za kwanza (Dubai I, Dubai II na Malaga) ndani ya mduara wa tano-bora.

Vijana wa Simiyu watasakata mchuano wa pili wa Kundi D dhidi ya Canada hapo kesho saa tano kasorobo asubuhi, na kufunga siku hiyo dhidi ya Scotland saa kumi na dakika 13.

Kenya ilipoteza 21-14 dhidi ya Australia makundini Dubai II mwezi Desemba.

Ikalimwa na Canada 19-17 katika Kundi D kalba kufinywa na Scotland 17-12 katika robo-fainali ya kuorodhesha nambari tisa hadi 16 mjini Malaga.

Hivyo ina kibarua inapolenga kulipiza kisasi.

Shujaa inakamata nafasi ya tisa kwa alama 23 baada ya kuzoa 10 Dubai I, 12 Dubai II na moja mjini Malaga.

Vincent Onyala, Herman Humwa, Billy Odhiambo na Alvin Otieno ni baadhi ya wachezaji watakaotegemewa zaidi na Shujaa kuepuka aibu nyingine.

You can share this post!

Balotelli atafaulu kuchezea Italia tena?

Jepkorir, Mateiko kuwa kivutio mbio za nyika za Discovery...

T L