Michezo

Kibera Blacks Stars yagonga City Stars

December 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KWA mara ya kwanza kwenye kampeni za kupigania taji la Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL), Nairobi City Stars iliteleza na kubugizwa bao 1-0 na Kibera Black Stars uwanjani Hope Center Kawangware, Nairobi.

Bao la pekee lililosaidia Kibera kuvunja rekodi ya kutofungwa ya City Stars lilifumwa kimiani na Janezz Oloo. Licha ya kichapo hicho, City Stars ya kocha, Sanjin Alagin ingali kileleni kwa kufikisha pointi 43 baada ya kuteremka dimbani mara 18.

Nayo Kibera ina alama 16 ikifunga 15 bora kati ya timu 20 zinazoshiriki ngarambe ya msimu huu wa 2019/2020.

Nayo Nairobi Stima ilishuka hatua mbili na kutua nne bora kwa alama 35 baada ya kupepetwa 3-0 Coast Stima yalifunikwa kimiani na Ombija Waithaka.

Bidco United ilirarua Fortune Sacco 3-0 na kurukia mbili bora kwa kuzoa pointi 36, moja mbele ya Vihiga United iliyovuna mabao 2-0 dhidi ya Mt Kenya United.

Nayo Ushuru ya kocha, James ‘Odijo’ Omondi iliandikisha ushindi mnono wa 4-1 mbele ya Maafande wa Kenya Police. Ushuru inazidi kushikilia sita bora kwa alama 29, sawa na Coast Stima.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Vihiga Bullets ilinyukwa 3-0 na Migori Youth, Shabana iliumwa 3-2 na FC Talanta. Nayo Muranga Seal ililipua Maafande wa Administration Police (AP) 4-1 huku Modern Coast Rangers ikitwaa 5-0 dhidi ya St Josephs Youth.