Kibera Ladies Soccer yatawazwa mabingwa wa Grandpa Super Cup

Kibera Ladies Soccer yatawazwa mabingwa wa Grandpa Super Cup

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kibera Ladies Soccer ilitawazwa mabingwa wa GrandPA Betika Super Cup baada ya kukung’uta Sunderland Samba kwa mabao 2-0 katika fainali iliyopigiwa uwanjani Impala Club Nairobi.

Kibera Ladies chini ya kocha, Davies Ikocheli na Cedric Mutiva ilionyesha soka safi na kunyamazisha wenzao ambao hushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza. Malkia hao walishusha ushindani mkali mbele ya wapinzani wao na kuhakikisha wametwaa taji hilo pale Anne Gorretty alipocheka na wavu mara mbili.

Nayo Uweza Women ilimaliza nafasi ya tatu baada kushinda wasomi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) kwenye mashindano hayo yaliokuwa ya makala ya pili. Kwenye nusu fainali ya ngarambe hiyo, Kibera Ladies Soccer ilinyanyua Uweza Women kwa mabao 2-1 huku Sunderland Samba ikiandikisha ufanisi wa mabao 3-0 mbele ya TUK

”Bila shaka tunafuraha kufuatia ushindi huo ambapo nilikuwa nikipima nguvu wachezaji wangu kwenye maandalizi ya kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu mpya,” kocha wa Kibera Ladies alisema na kuwataka wachezaji wake kuendeleza ubabe huo kwenye michuano ya ligi kupigania tiketi ya kurejea kushiriki kinyang’anyiro cha Ligi Kuu (KWPL).

Kwenye mashindano hayo Sylvia Akoth wa Sunderland Samba ilitwaa tuzo ya mfungaji bora alipotikisa wavu mara 11 tuzo ya mnyakaji bora ikimwendea Mercyline Akeyo wa Pegvision FC. Kibera Ladies itashiriki kampeni za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza baada ya kushushwa msimu uliyopita.

Victorina Ekwomo. wa Kibera Ladies Soccer akituzwa kombe la Grandpa Betika Super Cup…Picha/JOHN KIMWERE

”Tuna imani tunazidi kujipanga huku tukitarajia kufanya kweli kwenye kampeni za muhula huu na kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi,” kocha wa Kibera Ladies alisema huku akidokeza kuwa hawana sababu ya kutotimiza azma yao. Vipusa hao watashiriki michuano hiyo pamoja na Sunderland Samba, Limuru Starlets, Mombasa Olympic, Mukuru Talents Academy na Soccer Ladies kati ya zingine.

Kibera Ladies Soccer inajumuisha: Ruth Wanja, Zainab Khamis, Ruth Adhiambo, Ramadhan Fatma, Pauline Akinyi, Lilian Mboga, Lucy Achieng, Babe Achieng, Lucy Stella, Janet Mwangi, Millicent Okello na Victorina Ekwomo. Wengine wakiwa Diana Kaberere, Sheila Kwamboka, Cynthia Atieno, Anne Gorretty, Laventine Lihemo, Mercy Aluoch, Mercy Ochieng, Alice Wambui na Anne Waithera.

Mercyline Akeyo wa Pegvision akituzwa baada ya kuibuka mlinda lango bora kwenye mechi za Grandpa Betika Super Cup…Picha/JOHN KIMWERE

You can share this post!

Mashabiki waliopokea chanjo na ambao hawana virusi ndio wa...

Arsenal washauriwa kumuuza Aubameyang, kutafuta mvamizi...

T L