Michezo

Kibera Saints walenga ushindi

June 15th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

KIBERA Saints FC inasadiki kwamba imeketi mkao wa subira kupokezwa tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao.

Kikosi hicho ni kati ya timu 21 zilizokuwa zikishiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) kabla ya kupigwa stopu na kuzuka kwa janga la corona. Makocha wacho, Mark Tizodi na William Mulatya wanashikilia kuwa hakuna sababu ya kutopanda ngazi.

Makocha hao wamedokeza hilo baada ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kumaliza Ligi Kuu ya KPL kabla ya mechi kupigwa zote.

HUU NI MUHULA WETU

”Hatujacheza mechi zote za mkumbo wa kwanza ambapo tunalenga kupigana mwanzo mwisho tuhakikishe tumetimiza azma yetu,” alisema kocha Mulatya na kuongeza kuwa wana imani corona itaishi karibuni.

Kibera Saints yenye makazi yake katika mtaa wa Kibera, inaongoza katika jedwali la kipute hicho kwa kuzoa alama 35, moja mbele ya Kibera Soccer baada ya kucheza mechi 16 na 15 mtawalia.

Baadhi ya wachezaji wa KYSA Karengata.

Mwishoni mwa mwaka jana kocha huyo alinukuliwa akisema ”Huu ni muhula wetu wa kufanya kweli na kusonga mbele baada ya kushiriki mechi za ligi za viwango vya chini kwa zaidi ya miaka mitatu.”

Ili kukamilisha mechi 20 za raundi ya kwanza Kibera Saints itahitajika kutifua vumbi dhidi ya wapinzani wakuu, Kibera Soccer, Kibera Lexus, AFC Leopards na South B United.

Aidha amesema wachezaji wake wamo imara kujituma mithili ya mchwa huku wakilenga angalau kuzoa ushindi wa angalau wa mechi tatu kati ya hizo nne ili kufunga shughuli kiana.

Kadhalika kocha huyo alifunga kwamba bado hawajayeyusha malengo yao hasa kupigana kwa udi na uvumba kusaka tiketi ya kupandishwa daraja kushiriki kinyang’anyiro cha KPL ndani ya miaka minne ijayo.

Baadhi ya wachezaji wa WYSA United

KSG, WYSA UNITED

Kocha mkuu wa kikosi hicho, Mark Tizodi anakiri kwamba kama walivyotabiri mwanzoni mwa kipute hicho kamwe kampeni hizo hazikuwa mteremko.

Katika mpango mzima kwenye mechi zilizopigwa mapema mwezi Machi vikosi vya KSG na WYSA United viliandikisha matokeo ya kufana na kuonyesha wazi kwamba vilipania kufanya kweli.

Licha ya hayo endapo kipute hicho kitaamuliwa na matokeo ya mechi za mkumbo wa kwanza bila shaka vitaambulia patupu. Katika jedwali KSG imekamata nafasi ya saba kwa alama 27 sawa na WYSA United tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kwenye maandalizi ya kushiriki kampeni za msimu huu Saints ilitwaa huduma za vijana wanne wapya. Ilisajili Boaz Owino na Mulana Muoka (Kibera Azzuri) pia Kevin Omondi (GORP FC) na Cyrus Koroma raia wa Liberia.

Kadhalika ilinasa huduma zake Enock Omosa aliyekuwa akichezea Uweza FC kwa mkopo msimu uliyopita.