Makala

Kibera yafuta historia mbaya biogesi ya choo cha binadamu ikitumika kwa mapishi

February 21st, 2024 3 min read

NA LABAAN SHABAAN

MTAA wa Kibera umekuwa ukitambulika kwa sifa mbaya ya ‘urushaji’ wa choo ovyoovyo, hali iliyofanya wengi kuuita kama eneo la vyoo vya juu hewani almaarufu ‘flying toilets.’    

Dhana hiyo tata hurejelea vitendo vya watu kuenda haja katika vifurushi vya plastiki na kisha kutupa uchafu huo nje.

Lakini mambo yanabadilika kwa sababu mtaa huo umekuwa ukishuhudia maendeleo makubwa likija suala la usafi.

Wanamazingira na wadau wengine wanabadili uchafu wa binadamu kuwa tunu mbali na kusafisha mazingira.

Hili limewezeshwa na mpango shirikishi unaowahusisha wakazi, Wizara ya Afya na washikadau wengine.

Sasa choo cha binadamu kinabadilishwa kuwa kawi ya upishi shuleni na nyumbani.

Shule ya Tree Hill School ni makao ya kimojawapo cha vituo tisa vya kuzalisha biogesi kutumia kinyesi cha binadamu.

Vituo hivi vimesambaa Kibera tangu kufunguliwa mwaka wa 2022.

Mpango huu umepigwa jeki na Shirika la Maslahi ya Jamii la Umande Trust na washirika wengine pamoja na Shirika la Ufaransa kwa ajili ya ustawi.

Wakati wa chamcha, tunakutana na Gladys Njeri shuleni Tree Hill akiandaa chakula cha wanafunzi akitumia kawi hii.

Chakula kikipikwa kwa kawi ya biogesi. PICHA | LABAAN SHABAAN

Mapokezi ya uvumbuzi huu ni maendeleo kwa sababu mara tu baada ya kuanzishwa, wanajamii walichukia vyakula vilivyotayarishwa kutumia biogesi ya choo cha binadamu lakini baadaye wakakumbatia.

Baadaye, mapochopocho yaligeuka sumaku iliyowanasa wanafunzi kujisajili katika taasisi hii na hivyo kuongeza mahudhurio.

Ili kuongeza kukubalika, shirika la Umande Trust hufanya kampeni za uhamasishaji kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya gesi hii.

Awali, Junior Masinde, mhudumu katika kituo kimojawapo cha biogesi, alisita kujihusisha na upishi kutumia gesi hiyo.

Hakuwa na uhakika chakula kingekuwaje.

“Mwanzoni nilikuwa na wasiwasi kwamba chakula kingenuka kama kinyesi cha binadamu, lakini hali si hivyo na sasa nafurahia mlo unaopikwa hapa,” Masinde aliambia Taifa Leo.

Anaongeza, “Ni baraka zaidi ya maradufu. Tunasafisha mazingira, tunapata nishati safi na pia tunapata riziki.”

Vituo hivi huhudumia angalau watu 100 kila siku na walio shuleni huhudumia zaidi ya wanafunzi 150 kwa siku.

Msimamizi Mkuu wa Umande Trust Benazir Douglas anaarifu kuwa yeye hutamani kuona wakazi wa vitongoji duni wakiishi vyema. Yeye ni mvumbuzi aliyetunukiwa tuzo kwa kazi nzuri.

“Tulianzisha vituo hivi ili kuboresha viwango vyao vya usafi na kuunda njia ya kupata mapato kwa wanajamii wa makaazi duni.

Wanafurahia mapato kutokana na mauzo ya gesi safi na pia kutoza ada ndogo kwa wananchi wanaotumia vyoo hivi,’’ Benazir aliweka bayana.

Akizungumza na Taifa Leo, Rose Muthoni, mwalimu wa Shule ya Tree Hill iliyoko Laini Saba Kibera, alifichua kuwa mahudhurio hospitalini yamepungua baada ya usafi kudumishwa.

“Mwanzoni tulikuwa na vyoo viwili tu. Hii ilisababisha msongamano na kufanya unadhifu kuwa changamoto kwa watoto.

Wazazi waliogopa kuwaleta watoto wao katika shule hii sababu ya uchafu,” Bi Muthoni alikariri.

Karibu na lango la Shule ya Tree Hill, James Kariithi, muuza mboga, ni miongoni mwa wanaonufaika.

Bw Kariithi alieleza kufarijika kwake kutokana na upatikanaji wa vyoo vya umma katika eneo hilo.

“Mradi huu umeleta suluhu karibu na wananchi kwa kuwa tumekuwa tukijulikana kwa kuenda haja hadharani. Unasikia taarifa za ‘vyoo vinavyopaa’ kwenye vyombo vya habari tena?” aliuliza.

Hata hivyo, ongezeko la watu jijini limekuwa kizingiti kwa serikali kukabiliana na changamoto za usafi wa mazingira.

Hali hii inahitaji watu wabunifu kuibuka na uvumbuzi wa viwango vya juu.

Joe Okello, Afisa wa Afya ya Umma jijini Nairobi, anasema kuna mengi zaidi ambayo yanafaa kufanywa kudumisha usafi wa mazingira.

“Kuchimba vyoo vya shimo tu hakutoshi. Kwa hivyo, ili kufikia lengo hili, Kenya lazima itumie mbinu bunifu na kuhusisha jamii zilizoathiriwa,” alisema.

Upatikanaji wa maji safi hapa bado ni changamoto kwa hivyo tatizo hili hukwamisha utendakazi wa vituo vya kibiolojia.

Sensa ya 2019 ilifichua kuwa asilimia 7.4 ya vitongoji duni vinakosa huduma bora za vyoo.

Taswira hii husukuma takriban asilimia 10 ya watu kuenda haja hadharani.

Kwa kuwa taswira hii inatisha, hatua za pamoja zinahitajika ili kuleta mageuzi.

 

Mpishi wa shule, Bi Gladys Njeri, apakua chakula kilichopikwa kwa kutumia nishati safi iliyotengenezwa na choo cha binadamu. PICHA | LABAAN SHABAAN