HabariSiasa

Kibicho anavyotetemesha kambi ya Ruto

July 8th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

WASIWASI umekumba maafisa wa serikali na wanasiasa kuhusu uwezo mkubwa wa Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho wa kuvuruga Jubilee na urithi wa urais 2022, kutokana na mamlaka makubwa aliyo nayo.

Kulingana na duru miongoni mwa wanasiasa, mawaziri, makatibu wa wizara, wakuu wa usalama na utawala wa mikoa, Bw Kibicho kwa sasa ndiye mwenye mamlaka makubwa zaidi baada ya Rais Uhuru Kenyatta.

Katika taarifa ya majuzi ya polisi kuhusu maafisa ambao magari yao yanapasa kuondokewa barabarani, Bw Kibicho ni miongoni mwa waliowekwa katika ngazi ya kwanza pamoja na Rais, Naibu Rais na Mama Taifa.

Habari zinadokeza kuwa ameweza kujijenga kwa kupenyeza katika Ikulu, chama cha Jubilee, polisi, utawala wa mikoa, wizara zingine na mashirika. Hii imemfanya kuogopewa na hata wanasiasa wenye ushawishi mkubwa nchini.

TUMBO JOTO

Uwezo alio nao umemfanya kuzua tumbo joto katika kambi ya Naibu Rais William Ruto kwa kuwa ana nguvu kupindukia kiasi cha kuvuruga mipango yake ya kushinda urais 2022.

Katika wizara zingine mbali na yake ya Usalama wa Ndani, duru zinasema makatibu na mawaziri humshauri kila mara kabla ya kufanya maamuzi ya wizara zao. Magavana pia wanaripotiwa kutetemeshwa naye.

Maafisa wa ngazi za juu katika siasa na serikali waliambia Taifa Leo kuwa Bw Kibicho ndiye mtu anayetegemewa zaidi na Rais na kauli mbiu kwao ni kuwa: “Kibicho akiongea ni Rais amesema.”

Uwezo alio nao ni mkuu kiasi kuwa amemfunika Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua.

“Huyu ni Katibu ambaye ana nguvu nyingi kupindukia. Mamlaka yake yamevuka mipaka na sasa anatekeleza majukumu ambayo ni ya baraza la mawaziri,” asema mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi.

Tetesi za Bw Sudi zinatokana na hali kwamba Bw Kibicho hatishwi na mtu yeyote ndani ya serikali. Hali hii ilijitokeza wakati Bw Kibicho alipomwambia Naibu Rais awe akipiga ripoti kwa afisi yake anapoandaa hafla mashinani kama anataka kupewa ulinzi.

“Huyu ni Katibu ambaye akiamua kukuandama atakupata. Ana kila uwezo wa kuafikia anacholenga,” duru katika Wizara ya Usalama zinaeleza.

Taarifa ziliongeza kuwa katibu huyo ni mweledi katika kuvuruga wale anaotaka kumaliza kisiasa kwa kutumia vitengo vya usalama, utawala, wizara, mashirika ya serikali na hata mahakama.

“Huenda itatubidi katika Bunge kupiga msasa utendakazi na mamlaka anayotumia Bw Kibicho ili kujua kama ni halali, na iwapo anakiuka sheria achukuliwe hatua,” asema Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua.

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro anasema kuwa Bw Kibicho anasababisha uadui na migawanyiko ndani ya serikali kwa kuwa amenyakua majukumu hata ya kisiasa kutoka kwa wakuu wa Jubilee.

“Kibicho ndiye anayeamua mikutano ya kisiasa iwe ya akina nani na waongee kuhusu nini. Wikendi iliyopita tumemuona akiwakusanya baadhi ya wanasiasa wa Mlima Kenya kujadiliana kuhusu mwelekeo wa eneo la Kati kisiasa na kiuchumi. Wajibu wake si wa kisiaasa wala kimaeneo mbali ni kwa taifa lote na hivyo anakiuka mamlaka yake,” asema Bw Nyoro.

Anaeleza kuwa Rais Kenyatta amemwachilia sana Bw Kibicho kufanya atakalo, hali ambayo huenda akavunja Jubilee kama chama na serikali kwa jumla ikiwa hatathibitiwa.