Habari Mseto

Kibicho aonya wateketezaji soko Gikomba

June 26th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imetoa onyo kwa wahuni wanaohangaisha wafanyabiashara wa soko la Gikomba, jijini Nairobi kupitia mikasa ya moto inayoshuhudiwa mara kwa mara.

Onyo hilo lilijiri kufuatia mkasa wa moto uliozuka asubuhi ya kuamkia Alhamisi na kuteketeza mali ya thamani kubwa.

Kiini cha mkasa huo unaosemekana kuanza saa nane za usiku kimesalia kitendawili, lakini sehemu ya nguo na nafaka ndizo ziliteketea.

Cheche na ndimi kali za moto zilidhibitiwa mwendo wa saa tano za asubuhi kupitia vikosi vya pamoja vya wazimamoto, vilivyojumuisha wanajeshi waliotumia helikopta.

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho ameonya wanaosababisha mikasa hiyo ya moto Gikomba mara kwa mara chuma chao ki motoni.

Akizungumza alipofanya ziara katika soko hilo kutathmini hasara waliokadiria wafanyabiashara, Dkt Kibicho alisema ardhi ya Gikomba ni mali ya umma na kwamba haihusishwi kwa vyovyote vile na wawekezaji binafsi.

“Tunaonya wanaosababisha mikasa ya moto Gikomba. Ardhi ya Gikomba si ya kibinafsi, ni mali ya umma,” alisema.

Siasa, mivutano ya uongozi wa soko hilo na pia mizozano ya umiliki wa ardhi na vibanda, imekuwa ikitajwa kama kiini cha mikasa inayotokea.

Katibu Kibicho alitumia jukwaa la ziara hiyo kuweka wazi kuwa ardhi ya Gikomba ni mali ya umma.

“Hata tukihamishia wafanyabiashara katika soko mpya tunalojenga, ardhi ya Gikomba itasalia ya umma,” Dkt Kibicho alisema.

Februari 2020, mkasa mwingine ulishuhudiwa katika soko hilo. Aidha, kila mwaka Gikomba haikosi kushuhudia mikasa ya moto.

Ni matukio yanayoathiri kwa kiasi kikuu wafanyabiashara wanaotegemea Gikomba kujiendeleza kimaisha.

“Kabla ya wanaotuuzia kijumla kurejea walipokuwa, inachukua muda. Masoko na maghala yao yanapoteketezwa na moto, ni mavazi tunayonunua yanageuzwa kuwa majivu na ndimi za moto. Tunaathirika moja kwa moja,” mfanyabiashara anayepata nguo katika soko hilo Bw John Maina akaambia Taifa Leo.

Soko la Gikomba ni maarufu katika uuzaji wa bidhaa, hasa mavazi na viatu kwa bei nafuu, ambapo wafanyabiashara wengi nchini hulitegemea.