Habari Mseto

Kibicho, IEBC waagizwa kulipa familia Sh8m

February 25th, 2020 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA imemwagiza Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Marjan Hussein, kutoa ridhaa ya Sh8 milioni kwa msimamizi wa uchaguzi aliyeuliwa na polisi.

Msimamizi huyo aliuawa katika hali tatanishi.

Jaji Kanyi Kimondo alisema kuwa agizo hilo linatokana na uamuzi uliotolewa na mahakama ya Murang’a mnamo Aprili 26, 2018.

Familia ya msimamizi huyo, aliyetambuliwa kama Bw Waithanji Mwaniki, ilifika mahakamani ikitaka kulipwa ridhaa, kufuatia kifo chake nje ya kituo kimoja cha kupigia kura katika eneo la Kangema, Kaunti ya Murang’a kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

Marehemu aliajiriwa na tume hiyo kama Msimamizi wa Uchaguzi. Lakini mnamo Machi 4, 2013, alipigwa risasi na polisi wa utawala wakati alikuwa akisafirisha karatasi za uchaguzi kutoka Kituo cha Kupigia Kura cha Kiruri hadi katika Kituo cha Kuhesabia Kura cha Kangema.

Alifariki papo hapo katika kisa hicho kilichofanyika mwendo wa saa tisa usiku. Alipigwa risasi kichwani na polisi huyo kutoka nyuma. Walikuwa wamemaliza kuhesabu kura za Kituo cha Kupigia Kura cha Ichichi, kutia saini stakabadhi zote na kutuma matokeo.

Mahakama iliipa familia hiyo ridhaa ya Sh8.4 milioni, ambazo zingegawanywa kati ya wawakilishi wawili wa marehemu, waliotambuliwa kama Bi Benedditte Njeri na Bw John Mwitumi.

Baada ya kuongeza riba na gharama, IEBC na Wizara ya Usalama zilihitajika kulipa Sh4.4 milioni kila mmoja.

Hata hivyo, pande hizo zilichelewa kuzingatia agizo la mahakama, hali iliyoifanya familia kuandika barua kwa Mwanasheria Mkuu.