Michezo

Kibiwott Kandie amtumia salamu Joshua Cheptegei

October 8th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa kitaifa wa mbio za nyika, Kibiwott Kandie, amesisitiza kuwa analenga kumzidi maarifa mfalme wa dunia katika mbio za mita 5,000 Joshua Cheptegei ambaye ni raia wa Uganda, kwenye Nusu Marathon ya Dunia itakayoandaliwa mjini Gydnia, Poland mnamo Oktoba 17.

“Nimekuwa nikifanya mazoezi ya kutosha chini ya kocha wangu John Korir. Najihisi vizuri na niko tayari kumbwaga Cheptegei ambaye naamini atakuwa mshindani wangu mkuu,” akasema Kandie ambaye hushiriki mazoezi katika eneo la Ngong Hills.

Japo nguli wa riadha kutoka Ethiopia, Haile Gebreselassie, anampigia upatu Cheptegei kutamba katika mbio hizo za Poland, Kandie ameshikilia kwamba hana sababu yoyote ya kuhofia.

“Ni wakati tukiwa ugani ndipo tutajua kiwango cha maandalizi ya kila mwanariadha. Kwa sasa nalenga kuimarisha zaidi mazoezi yangu kwa wiki moja ijayo kabla ya kufunga safari ya kuelekea Poland,” akasema Kandie.

Kandie atalenga kuendeleza matokeo ya kuridhisha yaliyomshuhudia akiibuka mshindi wa RunCzech Half Marathon jijini Prague katika Jamhuri ya Czech mnamo Septemba 2020. Mwanariadha huyo alisajili muda bora wa dakika 58:38 kwenye kivumbi hicho.

Huu umekuwa msimu bora kwa Kandie ambaye pia aliibuka mshindi wa Ras Al Khaimah Half Marathon (RAK) mnamo Februari 2020. Mtimkaji huyo ataongoza kikosi cha wanariadha watano wa humu nchini wakiwemo Leonard Barsoton, Morris Munene, Bernard Kipkorir na Bernard Kimeli.

Kikosi cha wanawake kinajumuisha mshikilizi wa rekodi ya dunia kwenye mbio za kilomota 21, Peres Jepchirchir ambaye atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Joyciline Jepkosgei, Rosemary Wanjiru, Dorcas Jepchumba na Brilliant Jepkorir.

Kikosi cha Kenya kimeratibiwa kuondoka humu nchini mnamo Oktoba 15, 2020 na kinatazamiwa kuwasili Poland siku moja baadaye.

Naibu Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Paul Mutwii amesema washiriki wa mbio hizo za Poland wataendelea kujifanyia mazoezi kama awali.

“Hatutawaita kambini wanariadha watakaoshiriki Nusu Marathon ya Dunia. Badala yake, kila mmoja atashiriki mazoezi kivyake hadi Oktoba 14, 2020 ambapo watafanyiwa vipimo vya corona kisha kuelekea Poland siku inayofuata,” akasema Mutwii.

Mbio za Nusu Marathon ya Dunia zilikuwa awali zimepangiwa kufanyika Machi 29, 2020 kabla ya kuahirishwa na kuratibiwa upya kwa sababu ya janga la corona.