Kibomu cha Raila chatisha serikali

Kibomu cha Raila chatisha serikali

NA WAANDISHI WETU

UFICHUZI wa hivi majuzi kwamba huenda kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga alishinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, unaonekana kutetemesha viongozi wa Kenya Kwanza wanaomlaumu kwa vitisho.

Ufichuzi huo unaodaiwa kutolewa na mfanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), unaonyesha kuwa Bw Odinga alishinda uchaguzi huo kwa kura 8,170,353 ikiwa ni asilimia 57.3 dhidi ya Dkt William Ruto aliyepata kura 5,915,973 au asilimia 41.66 ya kura za urais.

IEBC ilimtangaza Dkt Ruto mshindi kwa kura 7,176,141 (asilimia 50.49 ) ya kura za urais zilizopigwa dhidi ya 6,942,930 (asilimia 48.5) za Bw Odinga.

Jana Jumapili, Azimio ilichapisha ufichuzi huo kwenye magazeti na leo Jumatatu, Bw Odinga anatarajiwa kufichua zaidi atakapohutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi.

Wiki jana, Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Jeremiah Kioni alisema Bw Odinga, aliyekuwa Afrika Kusini kwa wiki moja, atatoboa zaidi kuhusu ufichuzi huo akirejea nchini, hatua inayoonekana kuzua tumbojoto katika muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Wakiwa maeneo tofauti ya nchi jana, viongozi wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Rais William Ruto wametaja ufichuzi huo kama tabia ya Bw Odinga kuifanya nchi hii mateka wa siasa kupitia vitisho.

“Wakenya hawafai kuwa na wasiwasi. Sitaruhusu watu wachache kuingia katika kona fulani kupanga jinsi ya kututisha kupitia maandamano ili tuache kuzingatia huduma kwa Wakenya. Tunawaambia kwamba mwisho wao umefika. Ridhika na ulichopata kutokana na vitisho hivyo siku za mbeleni na utuache tuendelee kuhudumia Wakenya,” Dkt Ruto alisema akiwa Kaunti ya Kirinyaga.

Ingawa Bw Odinga ameandaa mkutano wa hadhara katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi, hajaitisha maandamano.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema anachofanya Raila hakiwezi kufaulu.

“Ni mbinu ya Raila Odinga ya kumfanya adumu katika siasa ambayo amekuwa akitumia lakini haiwezi kufaulu,” akasema Bw Gachagua.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano wa maombi uliohudhuriwa na Rais Ruto na Bw Gachagua, alisema hawatatishwa na mipango ya Raila.

Akizungumza akiwa Kakamega, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula alionya wanaotaka kufufua suala la matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 kuheshimu uamuzi wa IEBC na Mahakama na kuacha nchi kusonga mbele.

Akizungumza akiwa Nakuru ambapo aliungana na viongozi wengine kwa ibada ya Jumapili, Waziri wa Uchukuzi, Bw Kipchumba Murkomen alimtaka Bw Odinga kufuta mkutano wake wa leo Jumatatu katika uwanja wa Kamukunji.

Mbunge wa Ugenya David Ochieng alisema upinzani una machungu kwa kushindwa uchaguzini.

“Hawafai kuruhusu uchungu wa kushindwa kwenye uchaguzi kuvuruga kile Rais amepangia nchi hii,” alisema.

Iwapo madai ya Azimio ni kweli, basi kura za Bw Raila zilipungua kwa milioni 1.2 huku za Rais Ruto zikiongezeka kwa idadi sawa na hiyo.

Ripoti za Shaban Makokha, George Munene, Eric Matara na James Murimi

  • Tags

You can share this post!

Kaunti kufaidi mgao wa pesa za bandarini

Ajabu ya kanisa lililo na seli za kutesa waumini

T L