Habari Mseto

Kibomu chasubiri magavana wanaostaafu

May 29th, 2024 2 min read

Na COLLINS OMULLO

MAGAVANA ambao wamehudumu vipindi viwili na wanalenga kuwania nyadhifa nyingine sasa wako katika hatari ya kuzimwa kuwania kiti chochote cha kisiasa kwa muda wa miaka mitano.

Hii ni baada ya Bunge la Seneti kuidhinisha mswada unaolenga kuwazima magavana hao kuwania useneta, ubunge au udiwani baada ya kuhudumu kama gavana.

Kamati ya Sheria na Haki kwenye Seneti inayoongozwa na Seneta wa Bomet, Hillary Sigei, tayari imependekeza kuwa mswada huo uidhinishwe bila kufanyiwa marekebisho yoyote.

Uamuzi huo sasa unaiacha hatima ya magavana ambao wamemaliza muhula wao na wanalenga viti vingine ikining’inia padogo.

Mswada huo unaodhaminiwa na Seneta Raphael Chimera, unalenga kubadilisha Kifungu 180 cha Katiba kwa kuingiza sheria hiyo mpya.

Bw Chimera anasema magavana kuzuiwa kuwania wadhifa wa uongozi kwa kipindi cha miaka mitano, kunalenga kuhakikisha kuwa kukaguliwa kwa akaunti za kaunti kunakamilishwa na wanawajibikia hela zote walizotumia wakiwa afisini.

Ni baada ya ukaguzi huo wa matumizi ya pesa katika kaunti walizoongoza ndipo kutaamuliwa iwapo wamepita mtihani wa maadili na wanaruhusiwa kuwania vyeo vingine wakati wa uchaguzi.

Mwanasiasa huyo anasema kuwa magavana, wanapoendelea na majukumu yao, lazima wawajibikie mabunge ya kaunti na seneti kutokana na uamuzi wowote walioufanya.

“Hii sheria itahakikisha kuwa magavana wanawajibikia matumizi ya hela za kaunti,” akasema Bw Chimera.

“Vyombo na asasi zinazofuata matumizi ya pesa kwenye kaunti zitakuwa na muda wa kutosha kuzua maswali na kuwataka magavana hao wayajibu. Iwapo magavana watachaguliwa katika bunge, seneti au bunge la kaunti baada ya kuhudumu, watatumia nafasi zao za uongozi kuwavuruga magavana wanaohudumu na kutatiza uchunguzi,” akasema Bw Chimera.

Kwa sasa aliyekuwa Gavana wa Mandera, Ali Roba, na mwenzake wa Uasin Gishu Jackson Mandago wanahudumu kama maseneta. Wawili hao walihudumu kama magavana kati ya 2013 na 2022.

Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) imeunga mkono mswada huo, ikisema kuwa itasaidia kuzuia magavana kutumia mamlaka yao vibaya kwa kushiriki uporaji.

“Muda huo unatosha na utawazuia magavana wanaochaguliwa katika nyadhifa nyingine kuvuruga uchunguzi dhidi yao,” ikasema EACC ilipofika mbele ya kamati hiyo.

Hata hivyo, Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka (ODPP) imepinga mswada huo ikisema kuwa inavunja haki za magavana hao kuwania nyadhifa za uongozi ilhali katiba iko wazi katika suala la haki.

Baraza la Magavana Nchini (COG) nalo linasema kuwa marekebisho hayo ya kisheria yanaweza kutekelezwa tu kupitia kura ya maamuzi. COG inadai kuwa mswada huo unawahukumu magavana waliomaliza hatamu zao kwa kutegemea dhana kuwa walishiriki ufisadi.

“Mswada huo unaashiria kuwa magavana wanaomaliza hatamu zao wamepora pesa na kuzuia haki ya kila Mkenya ya kuwania kiti chochote cha kisiasa,” ikasema COG.