Habari Mseto

Mchapakazi Wilfred Kiboro aondoka Family Bank baada ya kuinua faida kutoka Sh526m hadi Sh2.5bn

May 28th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

BENKI ya Family imeagana na mwenyekiti wake wa bodi Dkt Wilfred Kiboro ambaye aliielekeza kuvuka vimbunga viwili hatari vya msukosuko wa sekta ya kifedha wa mwaka 2016 na janga la maradhi ya Covid-19.

Dkt Kiboro amekuwa katika wadhifa huo katika Family Bank tangu 2012 na akiondoka, anajivunia ufanisi wa kuifanya benki hiyo kuunda faida ya Sh2.5 bilioni baada ya kulipa ushuru katika mwaka wa 2023 ikiwa ni nyongeza ya asilimia 13.3 ikilinganishwa na mwaka wa 2022 ambapo faida ilikuwa ya Sh2.2 bilioni.

Dkt Kiboro aliingia kwa hatamu za uongozi wa bodi ya benki hiyo faida ikiwa Sh526 milioni na ambapo ameiacha ikiwa kwa kasi ya kuelekea kiwango cha Sh3 bilioni.

Katika tangazo rasmi la benki hiyo, Bw Francis Gitau ndiye atarithi mikoba ya Dkt Kiboro ili kuendeleza utendakazi ambao kwa sasa umeiweka ikiwa na biashara inayofikia kiwango cha Sh132 bilioni huku utajiri wake wote ukiwa ni wa Sh142.4 bilioni kutoka Sh128.5 bilioni mwaka 2022.

Dkt Kiboro anaondoka huku uwekezaji wa akiba wa wateja ukiwa katika kiwango cha Sh102.59 bilioni.

Tayari alikuwa ameweka mikakati ya kuzinduliwa kwa Wakfu wa Benki ya Family kwa lengo la kusaidia na kujihusisha vilivyo na masuala ya miradi ya kijamii.

Bw Gitau amekuwa mwanafunzi wa Dkt Kiboro kwa kipindi cha miaka tisa iliyopita alipojiunga na benki hiyo mwaka wa 2016 na akawa naibu mwenyekiti kuanzia mwaka wa 2022.

Dkt Kiboro ana ueledi wa kuongoza kampuni kubwa za uwekezaji, tayari akiwa mwenyekiti wa bodi katika kampuni ya Nation Media Group inayochapisha Daily Nation na gazeti la Taifa Leo.