Na WINNIE ATIENO
MWENYEKITI wa Benki ya Family, Wilfred Kiboro amewasihi viongozi wa dini kuhubiri amani na wanasiasa kukoma kuchochea Wakenya.
Aidha, Bw Kiboro alisema Kenya inapokaribia uchaguzi mkuu viongozi wa kidini na wanasiasa wanafaa wawe mstari wa mbele kuhubiri amani na utangamano.
Akiongea kwenye hafla ya kanisa la Presbyterian katika hoteli ya Milele, Kaunti ya Mombasa, Bw Kiboro alisema uchaguzi mkuu wa Agosti 9, haufai kutenganisha Wakenya.
“Tuko katika msimu wa siasa ambapo biashara huathiriwa na joto la kisiasa litakaloathiri sekta ya biashara. Lakini kanisa lina jukumu la kuhakikisha amani inadumishwa kwa kuihubiri,” alisema Bw Kiboro.
Bw Kiboro aliwataka Wakenya kuendelea kupendanana na kutobaguana sababu ya siasa. Kadhalika alisihi benki kusimama kidete na makundi ya kidini ili wawape mikopo ya maendeleo.