Habari MsetoSiasa

KIBRA: Kiyama cha Ruto, Raila chafika

November 6th, 2019 2 min read

Na CECIL ODONGO

UBABE wa kisiasa kati ya Naibu wa Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga utapimwa Alhamisi, wapigakura eneo la Kibra watakapofika debeni kumchagua mbunge mpya kutokana na kifo cha Ken Okoth miezi mitatu iliyopita.

Wawili hao waliendesha kampeni kali ya kuwavumisha wawaniaji wao na sasa mbivu na mbichi itabainika baada ya muda wa siku 21 wa kampeni uliowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(IEBC) kukamilika Jumatatu.

Kulingana na sajili ya IEBC, eneobunge hilo lina jumla ya wapigakura 118, 658 ambao wako katika wadi tano za Laini Saba (17,455), Lindi (16,688), Makina (25,695), Woodley/Kenyatta Golf Course (28,066) na Sarangombe 30,754.

Kulingana na IEBC, wapigakura wanatarajiwa kumiminika vituoni kuanzia saa kumi na mbili asubuhi huku shughuli za upigaji kura zikimalizika saa kumi na moja jioni.

Matokeo yatawasilishwa moja kwa moja kupitia njia ya kielektroniki kutoka kituo cha upigaji kura hadi kituo kikuu cha kujumuisha kura cha Chuo cha Mafunzo cha City Inspectorate, Dagoretti.

Kiti hicho kilichokuwa kikishikiliwa na marehemu Ken Okoth, kimewavutia wagombeaji 24, baadhi yao wakiwania kupitia vyama vya kisiasa na wengine ni wagombeaji huru.

Watakaojibwaga uwanjani kesho ni Khamisi Butichi wa chama cha Ford Kenya, Imran Okoth wa ODM, McDonald Mariga wa Jubilee, Eliud Owalo wa Ford Kenya, Anaciet Dorn (DP), Martin Andati (Modern Alliance Party), Ibrahim Kimorko (Roots Party), Kassim Abdul (The New Democrats) na Titus Mutinda (Republican Liberty Party).

Wengine ni Jared Nyakundi (National Liberal Party), Elijah Nyamwamu (National Rainbow Coalition -Kenya), Editar Ochieng (Ukweli Party), Emmanuel Owiti (Green Congress), Isaac Ogongo (Justice and Freedom party), Fransco Ojiambo (Party of Democratic Unity), Shem Ocharo (Munngano) na Hamida Musa (United Green Movement).

Wawaniaji huru ni Felix Anditi, Mathew Musyoka, David Odanga, Shedrack Omondi, Abraham Okoth na Noah Migudo.

Mwishoni mwa wiki jana, wanasiasa Bw Odinga na Dkt Ruto walikita kambi Kibra kuwavumisha wawaniaji wao, huku baadhi ya wadadisi wakisema kwamba ubabe kati ya wawili hao utatoa mwelekeo wa siasa za uchaguzi wa mwaka 2022.

Bw Odinga ambaye alihudumu kama mbunge wa Kibra kwa miaka 21, aliwaongoza viongozi na wanasiasa wanaounga mkono ‘handisheki’ katika uwanja wa Joseph Kang’ethe kumvumisha Bw Imran ambaye ni nduguye marehemu Bw Okoth huku Dkt Ruto na kundi lake wakifanya mkutano wao wa mwisho ugani DC.

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula pia walishiriki kampeni za kuwapigia debe wawaniaji wao.