Habari MsetoSiasa

KIBRA: ODM yaishtaki IEBC kuhusu sajili

November 5th, 2019 2 min read

Na MAUREEN KAKAH

CHAMA cha ODM kimeishtaki Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kukosa kuweka wazi sajili ya wapiga kura wa eneo bunge la Kibra.

Huku zikisalisia siku mbili pekee kufanyika kwa uchaguzi huo, ODM imeilaumu IEBC kwa kupanga njama ya kuwanyima haki wapiga kura wa Kibra kinyume na sheria.

Katika kesi hiyo iliofikishwa katika mahakama ya juu jijini Nairobi, ODM inadai kuwa kupitia barua kadhaa iliitaka tume hiyo ya uchaguzi kuweka wazi sajili ya wapiga kura lakini hawajatekeleza hilo.

ODM ilisema kuwa iliitumia IEBC barua katika tarehe tofauti za Septemba 20, Septemba 30 na Oktoba 2 lakini juhudi zao hazijazaa matunda yoyote kwani barua hizo hazikujibiwa.

Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Oktoba 3, IEBC iliahidi kutoa sajili hiyo kwa wakili wa ODM baada ya kulipwa Sh15,000.

Hata hivyo, baada ya chama hicho kuipitia sajili hiyo kiligundua kuwa sajili hiyo ilikuwa ni ile ambayo imetumika katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka wa 2017.

ODM ilisema mahakamani jana kuwa baada ya kujaribu kuitisha sajili ya sasa ambayo ingekuwa na data inayotarajiwa, IEBC ilidinda kuipeana.

Maelezo ya IEBC kuwa isingeweza kutoa sajili ambayo ina maelezo ya wapiga kura kwa sababu za kisheria, ODM ilisema kuwa madai hayo hayana msingi.

Kulingana na ODM, tume hiyo imekiuka sheria za kura ambazo zitapelekea kuwepo kwa kura za haki na za wazi.

“Kukataa kwa IEBC kutoa kwa nakala hiyo kunaonyesha njama fiche na hilo huenda likachangia kuwepo kwa ukora ambao utakuwa unatekelezewa wakazi wa Kibra kwa kuzuia watu wanaopaswa kupiga kura kutoweza kutekeleza hilo,” akasema wakili wa ODM Jackson Awele.

Mnamo Oktoba 25, IEBC ilitangaza kupitia gazeti rasmi la serikali kuwa kuna wapiga kura 118,658 ambao wamejisajili katika eneo bunge la Kibra. Notisi hiyo ya IEBC ilisema kuwa zoezi la kurekebisha sajili ya wapiga kura ilikuwa imekamilika.

Aidha, tangazo hilo pia lilionyesha kuwa kuna wapiga kura 17,455 katika eneo la Laini Saba, eneo la Lindi lina wapiga 16,688, Makina 25,695, Woodley/ Kenyatta Golf Course 28,066 na Sarangombe 30,754.

Vyama vya ODM, Jubilee, Ford Kenya na Amani National Congress (ANC) ni miongoni mwa vile ambavyo vipo na wagombeaji wa kiti hicho mbunge wa Kibra.

Wangombeaji hao ni pamoja na Bernard Imran Okoth wa ODM, McDonald Mariga wa chama cha Jubilee Khamisi Butichi kutoka Ford Kenya na Eliud Owalo kutoka ANC.