KIBRA: Tangatanga wadai wakuu walileta fujo

KIBRA: Tangatanga wadai wakuu walileta fujo

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Tangatanga wamemhusisha Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho kwenye fujo zilizoshuhudiwa eneo bunge la Kibra wiki jana.

Wakiongozwa na Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa, wabunge hao jana walidai kuwa siku moja kabla ya siku ya uchaguzi mdogo wa Kibra mnamo Alhamisi wiki iliyopita, Mbw Matiang’i na Kibicho walikutana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kupanga ghasia hizo.

‘Tuna habari kwamba Odinga, Matiang’i na Kibicho walikutana katika hoteli moja mtaani Karen kupanga namna wangetumia magenge ya wahalifu kusababisha fujo katika uchaguzi huo,’ akasema Bw Ichung’wa.

‘Tunajua kuwa magenge ya wahalifu waliowavamia wabunge Kibra walikuwa na ulinzi kutoka kwa watu wanaohudumu katika Afisi ya Rais,’ Bw Ichung’wa akaongeza kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Mbunge huyo alikuwa ameandamana na wenzake Caleb Kositany (Soy), David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki), Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Karatina), Japhet Mutai (Bureti), Kagongo Bowen (Marakwet Mashariki) na Jayne Kihara (Naivasha).

Hata hivyo, wabunge hao hawakutoa ithibati yoyote kuthibitisha madai yao, wakisema hawawezi kuandikisha taarifa kwa polisi kwa sababu hatua hiyo haina maana yoyote kwani hakuna hatua itakayochukuliwa dhidi ya watatu hao.

‘Tunamtaka Waziri Matiang’i atoe taarifa kuhusu uhalifu uliotendeka katika eneo bunge la Kibra. Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai pia aeleze hatua ambazo amechukua dhidi ya vijana waliowashambuliwa mheshimwa Didmus Barasa na seneta wa zamani Bonny Khalwale,’ akasema Bw Kositany.

Dkt Khalwale alinaswa katika kamera za vyombo vya habari akibeba mawe katika eneo la Kibera Lindi baada ya kufurushwa na vijana wa mrengo wa ODM.

Wabunge wengine waliofurushwa kutoka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura walikotumwa kuhudumu kama maajenti wa Jubilee ni Malulu Injendi (Malava), Oscar Sudi (Kapseret), Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) miongoni mwa wengine.

Jumanne, wabunge hao wa Jubilee walidai maafisa wa polisi waliotumwa kudhibiti usalama katika vituo vya kupigia kura hawakuchukua hatua yoyote kuwazima wahuni waliokuwa wakiwashambulia watu.

“Ilikuwa ni kana kwamba maafisa wa polisi walikuwa wamepokea maagizo ya kutoingilia kati magenge hayo ya vijana yakiwashambulia wabunge na wafuasi wetu, hali iliyopelekea wapiga kura wengine katika ngome zetu kutojitokeza kupiga kura,” akasema Bw Ichung’wa.

Wanasiasa hao sasa wanamtaka Bw Odinga kulaani fujo hizo na kuomba msamaha kwa wakazi wa Kibra na Wakenya kwa jumla.Mnamo Jumapili, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alisema chama hicho hakihusiani kwa namna yoyote na fujo zilizotokea siku ya upigaji kura mnamo Alhamisi wiki jana.

“ODM hakikuhusika na fujo wakati wa upigaji kura. Kile wafuasi wetu walifanya ni kulinda kura za mgombeaji wetu Benard Okoth Imran,” akasema Bw Sifuna wakati wa mkutano wa kusherehekea ushindi wa mgombeaji huyo.

Kufikia sasa Idara ya Polisi haijatoa taarifa yoyote kuhusu fujo hizo.

You can share this post!

Madiwani walia Joho amekuwa akiwahepa

KAULI YA MATUNDURA: Aina za udhibiti wa maandishi ya kazi...

adminleo