Michezo

Kibra United, Gogo Boys zalenga Ligi ya Taifa

December 10th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Kibra United iliendelea kuongeza kwenye kampeni za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili licha ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 na Gogo Boys  kwenye patashika iliyosakatiwa uwanja wa Briar Rose Academy School, Lang’ata jijini Nairobi.
Ni mchezo uliyosubiriwa kwa hamu na ngamu na wafuasi wa vikosi hivyo, ambapo pande zote zilishuka dimbani kutafuta pointi tatu muhimu. Kibra ya kocha,  Caleb Aringa ilifungiwa na Yusuf Alolo naye Collins Adapa aliibuka shujaa alipotikisa wavu mara mbili na kusaidia Gogo Boys kuzoa alama moja.
Kibra ilitoka nguvu sawa kwa mara ya pili mfululizo baada ya kutoka sare tasa na Korogocho Youth wiki iliyopita.
”Nashukuru vijana wangu kwa kujitahidi na kuzoa alama moja baada ya patashika hiyo kushuhudia ushindani wa kufa mtu,” kocha huyo wa Kibra alisema.
Baadhi ya wanasoka wa Kibra United ambao wanazidi kuwika kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula huu. Picha/ John Kimwere
Butterfy maarufu King of Ruiru ilipata ushindi wa kwanza baada ya kuzimwa mara tatu mfululizo ilipolaza Utafiti FC bao 1-0. Nahodha wa Butterfly, Evans Nakitare alichanja kona safi iliyochanganya mabeki wa Utafiti na kujifunga.
Kwenye matokeo, Kevin Wafula alicheka na wavu mara moja na kubeba CMS Allstars kugonga Ruiru Hotstars bao 1-0. Nayo Nyahururu Griffon ilibamiza Kariobangi Sharks B mabao 4-2.
Wafungaji wa Kariobangi walikuwa Daniel Karanja aliyepiga kombora mbili safi huku Patrick Mwangi na Joseph Mwangi waliitingia goli moja kila mmoja.
Kwenye jedwali, Kibra ikiwa kifua mbele ina alama 15, mbili mbele ya Gogo Boys.