Michezo

Kibra United yajilaumu kufuma mabao hewa

February 3rd, 2020 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MASHABIKI wa Kibra United waliondoka uwanjani wakinuna baada ya mvua kubwa kunyesha na kuvuruga mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili baina ya kikosi hicho na mahasimu wao Ruiru Hotstars iliyokuwa inaongoza bao 1-0.

Kibra ya kocha Caleb Aringa iliyotazamiwa kushinda mchezo huo na kuendelea kukaa kileleni ilijikuta pabaya baada ya kupoteza nafasi kadhaa katika kipindi cha kwanza na kuagana sare tasa.

Ruiru Hotstars ilipata bao hilo kupitia Benjamin Salim.

Kabla ya mchezo huo Kibra iliyokuwa inajivunia kutopoteza mechi yoyote ilikuwa kifua mbele kwa alama 23 sawa na wapinzani hao tofauti ikiwa idadi ya mabao.

”Kwa sasa hatujui itakavyokuwa baada ya mchezo wetu kutokamilika lakini hatuna shaka itabidi kujikaze kwenye mechi sijazo,” alisema mwenyekiti wa Kibra, Ibrahim Sebit.

Wanasoka wa Ruiru Hotstars kabla ya kushuka dimbani kucheza na Kibra United kwenye mechi ya Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili. Mchezo huo haukukamilika baada ya mvua kubwa kunyesha Ruiru Hotstars ikiongoza kwa bao 1-0. Picha/ John Kimwere

Nayo Gogo Boys ambayo ina mechi moja kapuni ilikomoa Butterfly maarufu King of Ruiru mabao 2-1 kupitia Hillary Shirao na Khubeiba Ali na kuendelea kufunga tatu bora kwa alama 21.

Naye Kevin Wafula aliibuka shujaa alipotingia CMS Allstars bao la pili dakika ya 90 na kuibeba kusajili ufanisi wa magoli 3-2 mbele ya Kariobangi Sharks B.

Wafula alitangulia kufunga dakika ya sita kabla ya Toure Simiyu kuongeza la pili dakika sita baadaye. Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, South B Sportiff FC ilizoa alama moja ilipoagana sare ya bao 1-1 dhidi ya Vision FC.

Butterfly iliyokuwa ikipigia chapuo kuwa miongoni mwa vikosi vitakaotesa wapinzani zaidi wapinzani wengine msimu ilijikuta njiapanda baada ya kupokonywa alama sita.

Kikosi hicho kiliangukiwa na adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kuvamia mwamuzi aliyekuwa akichezesha mchezo wao na Kariobangi Sharks mwishoni mwa mwaka jana.

Baada ya kisa hicho Butterfly FC imeshuka hadi nafasi ya sita kwenye jedwali.