Habari za Kitaifa

Kiburi, kejeli na majitapo yalivyochangia vijana kujibwaga barabarani kupinga Mswada wa Fedha 2024

Na MOSES NYAMORI June 26th, 2024 2 min read

KIBURI, uongo na majitapo ya viongozi wa Kenya Kwanza ni baadhi ya sababu ambazo zimewafanya Wakenya hasa vijana ambao hawana ajira, kujibwaga barabarani kujichukulia hatua mikononi mwao.

Baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu katika utawala wa Rais William Ruto wamekuwa wakiwakejeli raia wanaopitia nyakati ngumu za kiuchumi huku wao wakioneka kulewa mamlaka na kuishi kifahari.

Rais William Ruto aliingia mamlakani kwa ahadi ya kubuni nafasi milioni kadhaa za kazi kwa vijana. Pia aliahidi kuwa angewasaidia wale ambao wana mapato madogo kuinuka kiuchumi na kushusha gharama ya maisha.

Lakini miaka miwili baada ya kuwa afisini, Wakenya wameonekana kukerwa na kiburi cha Rais na maafisa wa ngazi ya juu katika serikali yake. Wengi wao wamekuwa wakiishi maisha ya kifahari, kuvaa mavazi ya bei ghali na kuwajibu Wakenya kwa kimadharau.

Baadhi ya wanasiasa ambao hawakuwa na hata chembe cha utajiri nao wanaonekana ‘wameomoka’ ghafla huku wakitoa hela nyingi tena za kustaajabisha katika michango ya Harambee.

Aidha kuna baadhi ambao wanahudumu serikalini ambao pia wameshangazwa na kiburi cha baadhi ya wandani wa Rais ambao hawaambiliki au kusemezeka kutokana na nyadhifa ambazo wanashikilia.

“Nawaomba wale ambao wapo serikalini ambao wamejaza matumbo yao wasiwatapikie wananchi. Komesheni kiburi, maringo na majivuno na mshughulikie changamoto ambazo zinawakabili raia,” akasema Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Raia ndio mabosi wao

Bw Gachagua ambaye kwa sasa hapatani na Rais aliwataka wanasiasa hao wakumbuke kuwa raia ndio mabosi wao kwa kuwa ndio waliwachagua katika kura ya 2022.

Kati ya wanasiasa ambao wanaonekana wamelewa mamlaka na wamekuwa wakiwapuuza vijana ni Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, Kiranja wa Wengi Silvanus Osoro, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot na wabunge Oscar Sudi (Kapsaret), Rachael Nyamai (Kitui Kusini), Gabriel Kagombe (Gatundu Kusini) na John Kiarie wa Dagoretti Kusini.

Mawaziri Alfred Mutua (Utalii) na Kipchumba Murkomen pia wamekuwa wakiwajibu vijana wanaoandamana kuhusu ushuru mwingi kwa kiburi huku wakionyesha ukwasi wao kwa kuvalia mavazi ya bei ghali.

Isitoshe, Mshauri Mkuu wa Rais Ruto kuhusu masuala ya uchumi David Ndii na Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura wamekuwa mstari wa mbele kuwajibu Wakenya vibaya kupitia taarifa za kiburi mitandaoni.

Tangu ajiunge na utawala wa Kenya Kwanza kama mshauri wa Rais kuhusu uchumi, Bw Ndii amekuwa akiwatusi mitandaoni Wakenya wanaouliza masuala yanayohusu matumizi ya fedha.

Aidha mara si moja ameonyesha kifua na kiburi kuhusu Wakenya ambao wanalalamikia mateso ya maisha magumu na ushuru ambao umewaathiri kibiashara.

“Kinaya ni kuwa vijana hawa ambao wanaandamana kupinga Mswada wa Fedha 2024 hawajui kile ambacho wanakifanya na ni watoto wa matajiri ambao wamewafilisi Kenya,” akasema Bw Ndii.

Bw Ichung’wah naye wiki jana aliwakejeli waandamanaji vijana, akisema hawakabiliwi na changamoto zozote na huletwa kuandamana kwa magari ya kifahari.

Msomi Profesa Macharia Munene naye amemrejelea Rais Ruto kama kiongozi anayejiamulia mambo wala hakubali kushauriwa kuhusu lolote na hata wandani wake.