Michezo

Kiburi kilivyomchimbia Mourinho kaburi

July 14th, 2019 2 min read

NA JOB MOKAYA

BAADA ya kupigwa kalamu miezi mingi iliyopita, Jose Mourinho bado anatapatapa hapa na pale akitafuta kazi. Kwa kawaida, kwa kocha mwenye haiba kama ya Mourinho, kupata timu nyingine ni sawa na papai kwa kijiko. Jambo dogo jepesi.

Makocha kama huyu huwa wamepata timu nyingine kabla hata ya kumaliza mkataba wao na timu walizonazo. Na endapo kazi itakwisha ghafla ilivyokuwa kwa Mourinho au hata kwa Arsene Wenger wa Arsenal, timu nyingi tena kubwa hupigana kutafuta saini yake.

Aliyekuwa kocha wa Chelsea Maurizio Sarri alipoondoka Chelsea, tayari Juventus ilikuwa karibu kunyakua saini yake. Zuri zaidi ni kwamba Juventus ilimnunua kocha huyu anayevuta sigara sitini kwa siku kutoka Chelsea.

Na kwa Mourihno, wala si sadfa hata kidogo. Ni kaburi la kujichimbia. Mtu aliyejawa na kiburi na majitapo kama Mourinho huwa haendi mbali. Angapaa juu afikilie mbingu, endapo atapaa na kiburi na majitapo, basi ataanguka kwa kishindo kikuu ardhini.

Sisemi kwamba Mourinho hatapata kazi. Lakini hata akipata, basi si ile ambayo angependelea. Juzi tu, Real Madrid imemfuta kocha wake. Yule Mourinho wa zamani angapata kazi hiyo mara moja. Sasa alipitwa na limbukeni Zinedine Zidane.

Juzi tena, si siku nyingi zilizopita, Juventus imemtimua kocha wake wa miaka mitani Massimiliano Allegri kwa madai ya kushindwa kunyakua taji la Klabu Bingwa barani Ulaya, yaani UEFA Champions League.

Mourinho yule wa zamani angEkuwa meneja sasa tena meneja wa Old Lady, kule jijini Turin, yaani Juventus. Kama wadhani napiga chuku kamuulize Chris Adungo, yule mchanganuzi maarufu wa soka wa Taifa Leo, au Sylvester Mukele, yule shabiki sugu wa Arsenal ambaye bado anasubiri taji la Ligi Kuu ya Uingereza.

Mourinho, yule wa kale, alitesa na kunyanyasa timu na mabodi ya timu waliotaka saini yake. Mourinho huyu wa leo anateswa na kunyanyaswa na mabodi yasiyomtaka karibu na nyuga zao. Ah! Mourinho.

Leo hii wakora wanaojiita makocha kama vile Sarri wanasakwa na kila klabu Ulaya. Sarri mwenyewe hajui wachezaji wake. Nani anacheza nafasi gani nani difenda, nani kiungo cha kati nani mtingaji. Yuko tu, na sigara zake. Jamaa anavuta pakiti tano za sigara uwanjani katikati ya mechi. Maneeeeeeeno hayo!

Tena yupo mwingine anayepiku Mourinho. Eti Mauricio Pochettino. Kwa ufupi, Pochettino anaifunza Tottenham Hotspur, timu ile anayoichezea Victor Wanyama. Hajawahi kushinda lolote la muhimu haswa taji la Ligi Kuu. Huyu pia yuko mbele ya Mourinho.

Mourinho, Mourinho! Tatizo liko wapi? Tatizo liko pale pale. Halijatoka. Kwamba, yeye huleta mgawanyiko mkubwa sana katika timu anapokaribia kutoka timuni. Wachejazi wengine wakiwa wamepondwa na kupondeka.

Akitoka Manchester United, alikuwa haongei na Paul Pogba, Antonio Valencia, Anthony Martial miongoni mwa wengine ambao siwezi nikawataja. Ndio maana hakuna timu yoyote inayomtaka Mourinho.