Habari MsetoSiasa

Kiburi kitakatiza ndoto yako ya Ikulu, Kuria amuonya Ruto

June 2nd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE mtatanishi kutoka Gatundu Kusini Moses Kuria amemkashifu Naibu Rais William Ruto kwa kuangazia maisha yake ya uchochole alipokuwa mtoto jinsi aliishi maisha ya umaskini.

Bw Kuria alimkosoa Dkt Ruto kuwa ameingiza majigambo baada ya kuingia uongozini na kumwambia kuwa safari ya maisha yake si tiketi ya kuingia Ikulu.

Mbunge huyo alisema pia naye alilelewa katika maisha ya kimasikini, lakini hawezi kutumia hali hiyo kujitafutia umaarufu.

“Kama mtoto wa masikini sitatumia hali kuwa nilizaliwa katika mazingira duni kama chombo cha kutafuta uongozi, jinsi tu sitarajii wale wa kutoka mazingira ya kitajiri kutumia maisha yao ya awali kama chombo cha kutafuta ama kuhifadhi uongozi,” Bw Kuria akasema katika akaunti yake ya Facebook.

Alitaja hali ya Dkt Ruto, ambaye Alhamisi katika hafla ya maombi ya kitaifa alieleza jinsi alikuwa masikini alipokuwa mtoto na sasa ana hadhi ya juu, kuwa kiburi ambacho hakitamfikisha popote.

“Majigambo hayakubaliki kwa wale wanaotoka kutoka mazingira ya kimasikini kama jinsi ilivyo kwa wanaotoka katika mazingira ya kitajiri,” Bw Kuria akasema.

“Upole unafaa kuwa kitu kinachotuelekeza tukiwa wauza kuku na watoto wa Marais,” mbunge huyo akasema.