Siasa

Kibwana anuia kusaka urais kwa tiketi ya KLM

November 17th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

GAVANA wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana, amepanga kutumia vuguvugu la Kongamano La Mageuzi (KLM) kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Vuguvugu hilo limepanga kutumia sikukuu ya Jamhuri Desemba 12, kutoa mwelekeo kuhusu nia yao kuunda serikali ijayo.

KLM ilizinduliwa miezi michache iliyopita likiwa na nia ya kuleta mageuzi ya uongozi nchini.

Prof Kibwana, jana alionekana kukashifu uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, pamoja na muafaka wa rais na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, almaarufu kama handisheki.

“Nimenuia kuwasilisha ombi la kuwania urais 2022 kupitia kwa vuguvugu la Kongamano La Mageuzi ifikapo Desemba 12. Kwa pamoja tutawakilisha Siasa Mpya badala ya siasa za handisheki wala tangatanga. Nitahitaji uungwaji mkono kutoka kwenu,” akasema gavana huyo, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

Hivi majuzi, Prof Kibwana alitangaza pingamizi zake dhidi ya ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Aliikosoa serikali ya Jubilee kwa kutotekeleza katiba iliyopo kikamilifu, na ukiukaji wa sheria kupitia bungeni.

Chini ya kanuni za KLM, mwanasiasa yeyote anayeweza kuthibitisha uadilifu wake atapewa nafasi kutumia vuguvugu hilo kushindania wadhifa wa kisiasa katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Vuguvugu hilo kwa sasa linajumuisha vyama vichache vya kisiasa na mashirika ya kijamii ambayo yanapigania uongozi bora.

Hata hivyo, waasisi wa KLM wanaojumuisha wanaharakati akiwemo aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, wamepiga marufuku wanasiasa ambao wamewahi kuhudumu kwa muda mrefu bila kuletea wananchi mafanikio au wale ambao wamewahi kutuhumiwa kwa madai ya ufisadi.

Mnamo Jumapili, vuguvugu hilo lilisema litakuwa na mkutano wa wajumbe siku ya Jamhuri ambapo viongozi wake watachaguliwa, na katiba yake kuzinduliwa.

Sawa na Prof Kibwana, wanachama wa KLM walikashifu mipango ya urekebishaji katiba kupitia kwa BBI.

Walikosoa pia Chama cha ODM wakisema kimesaliti Wakenya kwa kutetea misimamo ya serikali hata wakati mambo yanapoenda mrama.

“ODM inaendelea kupata mabilioni ya pesa za mlipa ushuru kwani ni chama rasmi cha upinzani ilhali kimekiuka wajibu wake. Chama hicho kimegeuka mtetezi mkuu wa misimamo ya utawala wa Jubilee,” wanachama hao wakasema kwenye taarifa.

Prof Kibwana anatumikia awamu yake ya pili ya ugavana ambao ni wa mwisho kikatiba.

Aliwania wadhifa huo kupitia Chama cha Muungano katika mwaka wa 2013, kisha mwaka wa 2017 akawania kupitia Chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka.

Katika eneo la Ukambani, wanasiasa wengine wanaopanga kuwania urais ni Bw Musyoka na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua.