Habari MsetoSiasa

Kibwana asifu madiwani wa Wiper waliompuuza Kalonzo

August 12th, 2019 1 min read

NA PIUS MAUNDU

GAVANA wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana, Jumatatu alizidisha uhasama wa kisiasa kati yake na Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka kwa kuwaunga mkono madiwani walioasi chama hicho na kuamua kushirikiana na serikali yake kinyume na agizo la kiongozi wao.

“Madiwani wa sasa wamefanya kazi nzuri. Wanafaa kuchaguliwa tena ili gavana atakayerithi nafasi yangu anufaike na uzoefu wao wa kutawala,” akasema Prof Kibwana Jumapili wakati wa hafla ya kuchangisha pesa katika kanisa la AIC Wote.

Prof Kibwana alisifu ushirikiano kati ya madiwani na serikali yake na akasema matunda yake yameonekana kutokana na maendeleo mengi yaliyoafikiwa na utawala wake.

Hii ilikuwa mara ya kwanza Prof Kibwana alikuwa akikutana na madiwani hao hadharani katika kipindi cha mwezi moja baada ya Bw Musyoka kuwazomea hadharani.

Bw Musyoka mwezi uliopita aliwalaumu madiwani waliochaguliwa kupitia Wiper kwa kushirikiana na serikali ya gavana huyo na kutotekeleza vilivyo majukumu yao ya ukosoaji.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Kiongozi wa wengi, Bw Kyalo Mumo ambaye pia ni diwani wa Tulimani alisema wataendelea kushirikiana na gavana huyo kwa maslahi ya wakazi wa Makueni wala hawatasukumwa na miegemeo ya kisiasa.

“Mapepo ya kishetani hayatafaulu kugonganisha bunge na serikali ya kaunti mara hii,” akasema.

Bunge la Kaunti hilo mwezi jana lilishuhudia vita vikali baada ya madiwani waaminifu kwa Bw Musyoka kulalamika kukandamizwa na utawala wa Prof Kibwana.

Madiwani hao wamekuwa wakizozana huku madai yakiibuka kwamba baadhi ya viongozi wenye ushawishi mkubwa eneo la Ukambani wamekuwa wakiwatumia kulemaza utendakazi wa kaunti.

Uhasama kati ya madiwani hao ulichangia uamuzi wa Bw Musyoka wa kutamatisha makubaliano ya kisiasa ya 2017 kati ya Wiper na chama cha Muungano kinachoongozwa na Prof Kibwana.