Siasa

Kibwana atangaza kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022

June 27th, 2020 1 min read

Na SAMUEL OWINO

GAVANA wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana anayehudumu kwa kipindi chake cha mwisho, anasema ameitikia mwito wa raia kuwa awanie urais mwaka 2022.

“Nimesikiza sauti ya ‘Wanjiku’ akiniomba niwanie urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Niko tayari kuwa Rais wa ‘‘Wanjiku’. Nitapambana hadi kwenye sanduku la kura. Ni lazima tuhakikishe kwamba ugatuzi unawanufaisha wananchi,” akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari ya Gavana huyo, Bw Edward Mwendwa baadaye kwenye taarifa, aliwahimiza Wakenya wamuombee gavana huyo, akisema uongozi wake utakuwa wa utumishi wenye nia ya kubadili nchi iwe kama ‘alivyoigeuza’ Makueni.

Tangazo la Prof Kibwana linamfanya awe wa pili kutangaza rasmi kuwa kwenye kinyang’anyiro cha urais, baada ya Naibu Rais William Ruto.

Aidha, hatua hiyo huenda ikaharibu hesabu za siasa za Ukambani, ikizingatiwa kuwa mshindani wake wa kisiasa, Kalonzo Musyoka huenda pia akawa na nia sawa na hiyo.

Wiki jana, Prof Kibwana alimaliza uhasama wake na aliyekuwa Seneta wa Machakos, Bw Johnstone Muthama, ambaye alitengana na Kalonzo na anatumikia adhabu kutoka kwa uongozi wa chama cha Wiper.