Michezo

Kichapo cha 2-0 chawaondoa Ushuru kileleni NSL

April 15th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TUMAINI la Ushuru FC kuendelea kukaa kileleni mwa kipute cha Supa Ligi ya Taifa (NSL) liligonga mwamba ilipozabwa mabao 2-0 na Shabana FC kwenye mechi iliyochezewa uwanjani Gusii mjini Kisii.

Wanasoka wa Kisumu Allstars walitwaa usukani wa michuano hiyo baada ya kujituma na kutia kapuni mabao 2-0 mbele ya Migori Youth

Nayo Nairobi Stima ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Green Commandos na kuendelea kufunga mbili bora kwa kufikisha alama 53, moja mbele ya Ushuru FC ya kocha Ken Kenyatta baada ya kupiga mechi 26 kila moja.

”Hakuna kulaza damu tunazidi kujituma kwa udi na uvumba kufukuzia ubingwa wa msimu huu na kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi,” alisema kocha wa Ushuru na kudai kwamba shughuli kamwe siyo rahisi.

Nacho kikosi cha Wazito kiligeuka na kuwa chepesi kilipofunikwa kwa mabao 2-0 na Eldoret Youth huku Coast Stima ikidhalilisha Kangemi Allstars kwa magoli 5-2.

Eldoret Youth inayoshiriki mechi hizo kwa mara ya kwanza ilivuna ufanisi huo kupitia Fredrick Obola na Amos Chingwa, naye Joe Waithira alitingia Wazito FC bao la kufuta machozi.

Kwenye mfululizo wa mechi hizo, Maafande wa Kenya Police walikomoa St Joseph’s Youth kwa bao 1-0, nayo City Stars ilibeba mabao 2-1 dhidi ya Modern Coast Rangers, Maafande wa Administration Police (AP) walitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Thika United huku FC Talanta ikiandikisha sare ya magoli 3-3 dhidi ya Fortune Sacco.