Michezo

Kichapo cha Jericho Allstars chaisaidi Meltah Kabiria

August 5th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

GITHURAI Allstars ililemea Jericho Allstars kwa goli 1-0 na kusaidia Meltah Kabiria FC na Mathare Flames FC kupunguza mwanya uliopo kati yao na wapinzani hao kwenye mbio za kipute cha Super Eight Premier League (S8PL) msimu huu.

Meltah Kabiria na Mathare Flames zilipiga hatua kwenye michuano hiyo baada ya kusajili ufanisi wa mabao 3-1 na goli 1-0 mbele ya Dagoretti Former Players na Lebanon FC mtawalia.

Githurai Allstars inayokuja kwa kasi kwenye migarazano hiyo ikiwa ndio mwanzo kushiriki ilishusha upinzani mkali mbele ya mahasimu hao na kuwazima kupitia goli lililojazwa kimiani na mcheka na nyavu bora Joe Abongo dakika ya 75.

”Katika mpango mzima tulipania kuwalima wapinzani wetu ili kulipiza kisasi baada ya kutuponda kwenye mechi za mkumbo wa kwanza,” kocha wa Githurai Allstars, Fredrick Ochieng na kuongeza kuwa bado hawajayeyusha matumaini ya kubeba taji hilo licha ya kudondosha pointi tatu waliponyukwa mabao 2-1 na Mathare Flames wiki iliyopita.

Kwenye patashika iliyoandaliwa Kawangware BP, Melta Kabiria ilikomoa wageni wao kupitia magoli ya Evans Vurugo, Javan Mukoya na Sammy Agesa baada ya kila mmoja kucheka na wavu mara moja.

Naye Victor John aliitingia Dagoretti Former Players goli la kufuta machozi. Naye Harun Omwenga alitikisa wavu mara moja dakika ya 21 na kubeba Mathare Flames ya kocha, Julius Katenge Mativo kunasa ushindi wa tatu mfululizo ilivuna goli 1-0 dhidi ya Lebanon FC .

Matokeo hayo yamefanya Jericho Allstars kujikuta njiapanda maana ingali kifua mbele kwa alama 36, moja mbele ya Melta Kabiria sawa na Mathare Flames tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Githurai Sportiff inafunga tatu bora kwa kukusanya alama 34, tatu mbele ya TUK ilitwaa mabao 3-1 dhidi ya NYSA.

MATOKEO YA MECHI ZA WIKENDI

Githurai Allstars 1-0 Jericho Allstars

Dagoretti F.P 1-3 Meltah Kabiria

Lebanon FC 0-1 Mathare Flames

Kawangware UTD 2-1 Makadara Junior S.A

NYSA 1-3 TUK

MASA 2-1 Shauri Moyo Sportiff

Team Umeme 1-3 Huruma Kona