Kichapo kutoka kwa Man-City hakina uwezo wa kuzima ari ya Liverpool EPL

Kichapo kutoka kwa Man-City hakina uwezo wa kuzima ari ya Liverpool EPL

NA CHRIS ADUNGO

INGAWA kichapo cha 2-1 ambacho Liverpool walipokezwa na Manchester City ligini Alhamisi iliyopita ni pigo kubwa, nahisi kwamba matokeo hayo hayatoshi kuzima ari ya kikosi cha kocha Jurgen Klopp kinachopania kunyanyua ubingwa wa taji la EPL msimu huu.

Ushindi wa Man-City haukuchangiwa kivyovyote na utepetevu wa Liverpool katika idara yoyote wala ukosefu wa kujiamini miongoni mwa wachezaji waliounga kikosi cha kwanza cha viongozi hao wa jedwali la Ligi Kuu.

Ilivyo, Liverpool walidiziwa maarifa na kikosi cha haiba kubwa ambacho kwa sasa ni miongoni mwa klabu bora za bara Ulaya.

Japo matokeo ya Liverpool dhidi ya Man-City yaliweka wazi kampeni za kuwania nafasi nne za kwanza kileleni mwa jedwali la EPL, Liverpool bado wanajivunia pengo la alama nne kati yao na Man-City baada ya kupigwa kwa jumla ya michuano 21 ligini.

Je, Manchester City wataweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza baada ya miaka 10 kutetea kwa mafanikio ubingwa wa EPL, au Liverpool watakomesha ukame wa miaka 29 wa taji la hilo kabatini mwao msimu huu?

Ingawa baadhi ya wadadidi wa soka wanahisi kwamba hii itakuwa ni zamu ya Tottenham Hotspur kutawazwa wafalme wa soka ya Uingereza kwa mara ya kwanza tangu 1961, wengi wanawapigia Liverpool upatu wa kutia kapuni ubingwa wa EPL muhula huu.

Hata hivyo, nahisi kwamba vikosi vya pekee vyenye uwezo wa kuvuruga matumaini ya masogora hao wa Klopp ni Man-City na Tottenham.

Licha ya kupoteza mchuano wao wa kwanza katika kampeni za EPL msimu huu, naamini Liverpool watajinyanyua na kuweka kando mikosi ya 2008-09 na 2013-14 ambapo waliongoza jedwali la EPL hadi mwanzoni mwa Mwaka Mpya kabla ya kupitwa na kuambulia nafasi ya pili mwishowe.

Katika misimu minane kati ya 10 iliyopita, klabu iliyokuwa ikiongoza jedwali la EPL baada ya kupiga nusu ya michuano yote ya msimu, ilitwaa ubingwa.

Baada ya kutinga fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu jana na kuanza kampeni za msimu huu wa 2018-19 kwa matao ya juu, Liverpool ni mpinzani ambaye kwa sasa amedhihirisha kuwa ana uwezo mkubwa usiostahili kupuuzwa.

Kikosi hicho cha Klopp kwa sasa ni timu tofauti kabisa. Viwango vya wachezaji wengi wa Liverpool vimeimarika kiasi kwamba uwepo wa Sadio Mane, Momahed Salah na Roberto Firmino kambini mwao unawafanya kuwa miongoni mwa klabu zinazojivunia safu bora zaidi za uvamizi.

Zaidi ya hayo, wanajivunia huduma za difenda Virgil van Dijk na nyani Alisson Becker ambao wanashikilia rekodi za kuwa beki na kipa ghali zaidi duniani kwa sasa. Hadi kufikia mwisho wa msimu uliopita katika EPL, Liverpool na Manchester United ndizo timu za pekee ambazo ziliishinda Man-City ligini.

Silaha kubwa ya Liverpool imekuwa ni uwezo wao wa kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza kupitia kwa wachezaji wao wenye kasi sana na ambao hawahitaji kupata nafasi nyingi za wazi ili wafunge mabao. Huu ndio upekee wa kikosi cha Klopp.

Kwa namna moja au nyingine, Liverpool ni timu ambayo ubora wake utadhihirika kila inapocheza na mpinzani aliye na mazoea ya kumiliki mpira kwa muda mrefu.

na ambaye anacheza soka ya kushambulia sana.

Mnamo 2013, Klopp aliwachochea Dortmund kutinga fainali ya UEFA baada ya kuwabandua Real Madrid kwenye nusu-fainali.

Ingawa kulikuwapo na klabu nyingi zenye vikosi bora zaidi kuliko Dortmund wakati huo, mfumo na upekee wa mbinu za ukufunzi wa Klopp uliwatambisha wapambe hao wa soka ya Ujerumani. Man-City na Liverpool kwa sasa ndizo timu zilizo na vikosi bora zaidi katika EPL. Hivyo, Liverpool kukomolewa 2-1 si kioja.

Muhimu zaidi ni kuyaweka kando maruerue hayo na kuendeleza ubabe wao kwa kuwa kutamatisha ligi bila ya kushindwa halikuwa mojawapo ya malengo yao makuu mwanzoni mwa msimu huu.

You can share this post!

Higuain mjanja wa kupiga chenga, hela zake zaweza kukausha...

ADUNGO: Nafasi ya lugha asili katika kusambaza tamaduni

adminleo